Friday, January 23, 2015

WANANCHI WA MAENEO YA MIRADI YA MAJI WATAKIWA KUTOZEMBEA KUJADILI MAENDELEO YA MIRADI

unnamed (68)Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza akiwakaribisha wajumbe wa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji waliotembelea mkoa huo kukagua baadhi ya miradi ya Maji iliyopo mkoani humo.
unnamed (70)Kiongozi wa ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Amina Makilagi akieleza lengo la ziara ya kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji mkoani Mtwara kwa Mkuu wa mkoa huo Mwantumu Mahiza (kushoto). Kulia ni mjumbe wa kamati hiyo Asaa Hamadi.
unnamed (71)Mwenyekiti wa Halmashauri ya Lindi Mathei Makwinya, akieleza jambo wakati ziara ilipowasili kwenye kijiji cha Mnara kukagua mradi wa Rondo-Mnara. Kulia kwake ni Kiongozi wa wajumbe wa kamati ya Bunge, Amina Makilagi, Mkuu wa wilaya ya Lindi Nassor Himid na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Lindi Olliver Vavunge.
unnamed (72)Baadi ya viongozi wa kijiji na kamati ya maji ya kijiji cha Mnara na Chiponda wakimsikiliza Kiongozi wa ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Amina Makilagi (hayupo pichani).
unnamed (74)Kiongozi wa ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Amina Makilagi, akizungumza na viongozi wa mradi wa maji wa Rondo-Mnara na kata ya Mnara.
unnamed (75)Mhandisi wa Maji mkoa wa Lindi Valentine Ndyano (aliyevaa shati la kitenge) akifafanua jambo kwa wajumbe wa kamati ya Bunge kuhusu mtambo wa kusukuma maji.
unnamed (77)Mhandisi wa Maji mkoa wa Lindi Valentine Ndyano akifafanua jambo kwa wajumbe wa kamati ya Bunge kuhusu mtambo wa kusambaza maji kwenye vituo vya maji.
unnamed (78)Kiongozi wa wajube wa kamati akizingumza na wananchi wa kijiji cha Mnara baada ya kukagua mradi wa maji wa Rondo-Mnara.unnamed (80)Wajumbe wakikagua maendeleo ya mradi huo unaotarajiwa kukamilika Machi mwaka huu.
…………………………………………………………………….
Hussein Makame, MAELEZO, Lindi
WANANCHI waliopo kwenye maeneo ya miradi ya maji mkoani Lindi na nchini kwa ujumla wametakiwa kuacha kuzembea kwenye vikao vya kujadili maendeleo ya miradi hiyo kwani kufanya hivyo kutachangia kufa kwa miradi hiyo.
Hayo yamesemwa na Kiongozi wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji mkoani Pwani, Lindi na Mtwara Amina Makilagi (Mb) wakati alipotembelea mradi wa maji wa Rondo-Mnara uliopo katika kijiji cha Mnara Kata za Mnara na Chiponda wilaya ya Lindi mkoani Lindi.
Alisema miradi mingi ya maendeleo imekufa kutokana na wananchi kuzembea kwenye vikao vya kujadili uendeshaji wa miradi ya maji, hivyo kuwafanya viongozi wasio waaminifu kutumia vibaya fedha za miradi hiyo.
“Mnachotakiwa msizembee kwenye vikao vya kujadili miradi ya maji kwani mkifanya hivyo miradi itakufa kutokana na viongozi kutumia vibaya fedha za miradi hiyo kujinufaisha wenyewe” alisema Makilagi.
Alisema wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanasimamia utaratibu wa kuingiza fedha za miradi ya maendeleo ya maji kwenye akaunti kwani kufanya hivyo kutaepusha viongozi wabadhirifu kuihujumu miradi hiyo.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya wajumbe wa kamati hiyo ya bunge, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Lindi Olliver Vavunge alisema mradi wa Rondo-Mnara ulisanifiwa kuhudumia wakazi 18,000 kwenye vijiji sita.
Alisema mradi huo uliojengwa na serikali mwaka 1973 una uwezo wa kuzalisha mita za maji zenye ujazo wa 450 kwa siku lakini kutokana na changamoto ya uchakavu wa mitambo na gharama kubwa za uendheshaji, uzalishaji umepungua hadi mita za ujazo 328 kwa siku.
“Vituo vitatu vya kusukua maji vilijengwa kutoka kwenye chanzo cha maji kilichopo katika kijiji cha Chikote.Ambapo kwenye kila kituo ilifungwa mitambo miwili ya kusukuma maji iliyotumia injini ya diseli.” Alisema Vavunge.
Alisema mradi wa Rondo-Mnara ni miongoni mwa miradi minne ya maji safi na salama ambayo hadi sasa imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi ikiwemo miradi ya Kiwawa, Likwaya na Namkongo.
“Miradi hiyo inatoa huduma ya maji kwa wakazi 5,000 huku halmashauri ikiendelea kutekeleza miradi ya Maji ya Namangale, Hingawali, Littipu, Nyangamara na Nahukahuka” alisema.
Kwa upande wa mradi wa Ng’apa unaojulikana kwa jina la 7 Towns Upgrading Program, unaofadhiliwa na serikali ya Ujerumani na Jumuiya ya Ulaya, una lengo la kuboresha huduma ya maji katika mji wa Lindi.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka huu na kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi 194,143 wa manispaa ya Lindi na unajenga mtambo wa kusafisha majitaka yanayozalishwa katika mji wa Lindi.
Awali akiwasilisha taarifa ya huduma ya maji mkoa wa Lindi kwa wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge mkoani Lindi, Afisa Tawala wa Mkoa wa Lindi Abdallah Chikota alisema hadi Novemba mwaka 2014 wakazi wa mijini wanaopata maji safi ni asilimia 55.4 ya wakazi wote 162, 049.
Alisema kwa upande wa wakazi wa vijijini wanaopata huduma ya maji safi na salama wanakadiiriwa kufikia 297,796 kati ya wakazi 702, 603 wa vijijini.
Naye Mkuu wa mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza alisema pamoja na Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa mkoa huo, lakini huduma hiyo haipatikani kama inavyotakiwa kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme ambao kwa siku unaweza kukatika kati ya mara 22 hadi 25.
Hata hivyo, alisema amewasilisha taarifa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na wanatarajia kukutana na uongozi wa juu wa shirika hilo hivi karibuni ili kujadili changamoto hiyo ambayo inategemewa kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji mkoani humo.
Ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji inaendelea kukagua miradi ya maji katika mkoa wa Mtwara ambapo inatarajia kukagua miradi ya Nanyamba-Namkuku na Tandahimba-Matogolo.

No comments: