Thursday, April 03, 2014

MSTAHIKI MEYA WA MANISPAA YA ILALA JERRY SILAA AGAWA DAWATI 300 KWA SHULE ZA SEKONDARI MANISPAA YA ILALA

DSC_0622
Mstahiki Meya Jerry Silaa akiteta jambo na mmoja wa wanafunzi wa kidato cha tatu ambaye ni mlemavu Voster Peter wakati akikabidhi madawati shuleni hapo.
DSC_0428
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, ambaye pia ni Diwani wa kata ya Gongo la Mboto Jerry Silaa akiwasili kwenye shule ya sekondari Pugu kwa ajili ya kukabidhi madawati 300 kwa shule tatu zilizopo manispaa ya Ilala na kulakiwa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Jovinus Mutabuzi.

.Ni katika Mpango wa “Mayor’s Ball” “Dawati ni Elimu, Kalisha mmoja, boresha Elimu”.

Na Zainul Mzige
“Kiongozi hapaswi kutegemea nguvu za Serikali kufanya shughuli za maendeleo” Hayo ni maneno ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala ambaye pia ni Diwani wa kata ya Gongo la Mboto, Jerry Silaa katika hafla ya kukabidhi madawati kwa shule tatu za sekondari zilizopo Manispaa ya Ilala iliyofanyika Shule ya sekondari Pugu.

Katika hafla hii, jumla ya madawati 300 yenye thamani ya shilingi milioni 45 za kitanzania yaligawiwa kwa shule 3 zilizopo manispaa ya Ilala ambazo ni Shule ya sekondari Pugu (107), Shule ya sekondari Ulongoni (93) na Shule ya sekondari Jangwani (100) kupitia jitihada zake za kuanzisha mpango wa Mayor’s Ball 2013 ulioanza mwaka jana kupitia kampeni ya “Dawati ni Elimu, Kalisha mmoja, boresha Elimu”.

Bwana Silaa alitoa pongezi na shukrani za dhati kwa wote waliotimiza ahadi zao katika kufanikisha zoezi zima la ununuzi wa madawati mapya na kufanikisha kampeni yenye lengo la kuinua viwango vya elimu ya sekondari na msingi Tanzania. Pia, alichukua nafasi kuwaomba wadau waendelea kujitokeza kuchangia elimu kwani ni mara ya kwanza kwa jambo hili la “Mayor’s Ball” kufanyika nchini.
DSC_0431
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa, akisaini kitabu cha wageni katika shule ya sekondari Pugu mara baada ya kuwasili shuleni hapo.

“naomba nitumie nafasi kuwapongeza wadau wote walioitikia wito huu na naomba kutoa rai kwa wale wote walioahidi kutimiza ahadi zao ili kufanikisha lengo la kampeni hii iliyobeba kauli mbiu ya Dawati ni Elimu kalisha mmoja, boresha elimu”, alisema Mstahiki meya Jerry Silaa.

Katika hotuba yake, amewaasa wanafunzi kusoma kwa bidii hasa baada ya kuwaboreshea mazingira ya kusomea kwa msaada wa madawati mapya na ya kisasa.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Gongo la Mboto, Imelda Samjela, ameiomba serikali kuu kuiangalia shule ya Sekondari Pugu kwa jicho la pili kutokana na hadhi yake ya kutoa viongozi nchini na kuifanya iwe na hadhi ya kimataifa. Shule ya sekondari Pugu inajivunia sifa ya kuwa shule iliyozaa viongozi shupavuTanzania akiwemo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Bi. Imelda aliongeza kuwa kila mwaka tunapoadhimisha Maisha ya Mwalimu Nyerere basi kufanyike jambo aidha kupaka rangi na kusafisha mazingira ya shule hiyo iliyobeba historia ya Taifa la Tanzania. Diwani pia alitoa wito wa kuweka fungu la fedha za kukarabati majengo ya shule hiyo pamoja na kutokomeza kero ya Kunguni shuleni.
DSC_0446
Mwalimu Mkuu wa Shule ya sekondari Pugu, Jovinus Mutabuzi(mwenye suti nyeusi) akizungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo mbele ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa. wengine pichani ni wakuu wa shule za sekondari Ulongoni na Jangwani waliojuika katika hafla hiyo ya kukabidhiwa madawati.

Kunguni wamekuwa ni kero kubwa kwa wanafunzi hasa wakati wakulala. Alitoa angalizo hili kwa mwenyekiti wa huduma za jamii.

Akitoa ufafanuzi wa suala la ukarabati wa majengo ya shule hiyo, Mwenyekiti wa huduma za Jamii Manispaa ya Ilala, Bi. Angelina Nalembeka amesema kuwa Manispaa ilishatoa shilingi Milioni 50 kwa ajili ya ukarabati na wanampango endelevu wa kufanya hivyo kila mwaka. Mpango huu si tu kwa shule ya Pugu bali kwa shule nyingine pia zinazoizunguka manispaa ya Ilala

Mwenyekiti huyo pia alithibitisha kufanyika kwa zoezi la awali la kutokomeza Kunguni shuleni kwa kunyunyiza dawa na kuwepo kwa mpango endelevu wa kunyunyiza dawa ili kuondoa kabisa kero hiyo ya Kunguni shuleni.
DSC_0456
Mstahiki Meya Jerry Silaa akipitia moja ya mafaili ya taarifa za shule hiyo.
“Mheshimiwa Diwani amefuatilia suala lenu la Pugu kwa umakini na taarifa zake tunazo katika Halmashauri. Mwalimu mkuu atakuwa shahidi na tumeshakuja kupiga dawa na bado mwaka huu tutakuja kupiga dawa tena kuondoa Kunguni” alisema Mwenyekiti, Huduma za Jamii.

No comments: