Serikali imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 111 kununua mazao kwa wakulima katika kipindi cha mwaka 2013/2014 ikiwa ni malipo kwa wakulima baada ya kuiuzia nafaka Serikali.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Bw. Charles akiongea na waandishi wa Habari( Hawapo Pichani) kuhusu mafanikio yaliyopatikana na wakala hao ikiwamo kutumia Zaidi ya Bilioni 111 kununua mazao kwa wakulima katika kipindi cha Mwaka 2013/2014. wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mipango na Uendeshaji wa wakala huo Bi. Anna Mapunda.
Baadhi ya waandishi wa Habari waliohudhuria Mkutano huo wakimsikiliza Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Bw. Charles wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar es Salaam.
Picha na Georgina Misama
--
Na Frank Mvungi
SERIKALI imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 111 kununua mazao kwa wakulima katika kipindi cha mwaka 2013/2014 ikiwa ni malipo  kwa wakulima  baada ya kuiuzia  nafaka Serikali.

Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Charles Walwa wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari jana jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akieleza mafanikio yaliyofikiwa na  wakala huo.
Walwa alisema kuwa wakala huo umeweza kuongeza kiasi cha nafaka zilizonunuliwa kutoka kwa wakulima kutoka  tani 61,587.784 mwaka 2008/2009 hadi tani 219,377.282 mwaka 2013/2014 ikiwa ni matokeo ya kuboreshwa kwa mifumo ya utendaji wa wakala huo.

“Hadi kufikia Desemba 31 mwaka 2013 wakala ulinunua tani 219,377.282 za nafaka sawa na asilimia 110 ambapo tani 218,878.600 ni mahindi na tani 498.682 ni mtama” alisema Walwa.

Aliongeza kuwa wakala umeingia makubaliano ya mashirikiano ( Memorandum  of Understanding(MOU)  na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ili kuwahakikiishia wakulima soko la uhakika.

Katika kutekeleza makubaliano  na WFP  Walwa alisema kuwa wakala umeuza tani 80,000 mwaka 2011/2012 ambapo kwa sasa wakala unaendelea kutekeleza mkataba mwingine wa kuuza tani 23,000 kwa mwaka 2013/2014.

Katika hatua nyingineWalwa alisema kutokana na mfumo mzuri wa manunuzi ya nafaka kutoka kwa wananchi,  ajira za muda kwa wananchi takribani 3000 zizizalishwa na makundi mbalimbali ya wananchi wakati wa kukusanya nafaka tatika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula umepanga kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 241,000 za Sasa hadi tani  laki 400,000 ifikapo mwaka 2016 na Tani 700,000 ifikapo mwaka 2024

Comments