WAZIRI MEMBE KUPOKEA TUZO YA AFRICA’S MOST IMPACTFUL LEADER OF THE YEAR KWA NIABA YA RAIS KIKWETE


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atapokea tuzo ya Africa’s Most Impactful Leader of the Year kwa niaba ya Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania mjini Washington D.C, Marekani tarehe 09 Aprili, 2014.
Tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka na Taasisi ya Uchapishaji ya African Leadership Magazine yenye makazi yake nchini Marekani kwa viongozi wa Afrika wanaofikia vigezo vilivyowekwa na Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia utawala bora, demokrasia na kuheshimu haki za binadamu kwa Mwaka 2013 inatolewa kwa Mhe. Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa Taasisi ya African Leadership Magazine, Tuzo hiyo inatolewa kwa Mhe. Rais Kikwete kutokana na namna ya pekee ya uongozi wake wenye matokeo yanayopimika kiutawala bora hususan kwa mwananchi wa kawaida wa Tanzania. Aidha, uongozi wake umeiletea Tanzania heshima kubwa kimataifa na kuiweka Tanzania kama chaguo muhimu kwa wawekezaji kutokana na ukuaji uchumi na maboresho ya sera.
Tuzo hiyo tayari imewahi kutolewa kwa Marais na Viongozi wengine mbalimbali wa Afrika wakiwemo Mhe. Ellen Johnson Sirleaf, Rais wa Liberia, Mhe. James Michel, Rais wa Shelisheli na Rais Mstaafu wa Ghana, Mhe. John Kuffor.
Ujumbe wa Mhe. Membe utamhusisha Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Salvatory Rweyemamu, Waandishi wa Habari na Maafisa wa Serikali. Mhe. Membe atarejea nchini tarehe 11 Aprili, 2014.

Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
8 APRILI, 2014

Comments