Thursday, April 24, 2014

TACAIDS yadhamiria kuanzisha Mfuko wa Ukimwi utakaolenga kuondoa upungufu wa Rasilimali katika maeneo mbalimbali ili kuboresha afua za ukimwi nchini.


Mkurugenzi wa Sera, Mpango na Utafiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dkt. Raphael Kalinga akiwaeleza jambo waandishi wa Habari( Hawapo pichani) Wakati wa Mkutano ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO)  Jijini Dar Es Salaam.Kushoto ni Afisa Habari Mkuu wa Tume Hiyo Bi. Nadhifa Omar.

-----

Na Hassan Silayo-MAELEZO

Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imedhamiria kuanzisha Mfuko wa Ukimwi utakaolenga kuondoa upungufu wa Rasilimali katika maeneo mbalimbali ili kuboresha afua za ukimwi nchini.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Sera, Mpango na Utafiti wa Tume hiyo Dkt. Raphael Kalinga jana Jijini Dar es Salaam.


Dkt. Kalinga alisema kuwa uanzishwaji wa Mfuko huo ni moja yakipaumbele kilichowekwa na Tume hiyo katika kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa mkakati wa taifa wa kudhibiti Ukimwi  kwa mwaka wa Fedha 2014/2015.


“Katika kuendelea kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa mkakati wa taifa wa kudhibiti Ukimwi  kwa mwaka wa Fedha 2014/2015 Tume imeamua kuweka vipaumbele ikiwamo kuanzisha mfuko wa UKIMWI( ATF) utakaolenga kuondoa upungufu wa Rasilimali katika maeneo mbalimbali ili kuboresha afua za ukimwi nchini” Alisema Dkt. Kalinga.


Aidha Dkt. Kalinga aliongeza kuwa mfuko huo unategemewa kuaza ifikapo Julai, 2015 na kuanza jukumu la kuhamasisha utafutaji wa Rasilimali za kudhibiti Ukimwi Nchini.


Pia Dkt. Kalinga alibainisha kuwa Tume itaendelea kutoa kipaumbele cha afua za Vijana hasa walio katika umri kati ya miaka 15 hadi 24 waliopo shuleni na nje ya shule kwa kuwa ndio kundi lenye changamoto ya rika balehe na pia ufahamu mdogo ambao ni sawa na asilimia 40.3 kwa wanawake na 47.3 kwa wanaume kwenye masuala ya ukimwi.


Pia Dkt. Kalinga aliongeza kuwa kundi hilo halina hamasa hasa katika masuala ya upimaji wa Ukimwi na Matumizi ya kinga, baadhi wanajihusisha na tabia hatarishi ikiwamo kujiunga na makundi hatarishi, wanachangia kwa asilimia kubwa maambukizi ya ukimwi kulingana na utafiti wa viashiria vya ukimwi na malaria wa Mwaka 2011/2012.


TACAIDS imepanga kuhamasisha Halmashauri zote nchini kutenga fedha za udhibiti UKIMWI kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya Ndani.

No comments: