Thursday, April 03, 2014

Soma Taarifa Maalum Kwa Umma ya Ufafanuzi Kuhusu Tume ya Katiba:Kutupiwa Virago:Kiinua Mgongo Millioni 200 Kwa Kila Mjumbe


Gazeti la Raia Mwema lililotoka leo, Jumanne, Aprili 2, 2014, limeandika habari zisizokuwa za kweli chini ya kichwa cha habari : “Warioba: Ikulu imetutupia virago”
Habari hiyo inamkariri aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba akidai kuwa Tume yake ilifukuzwa kazi, kwamba haikupewa muda wa kuandaa na kuwasilisha nyaraka za kukabidhi ofisi na madaraka na kwamba wajumbe wa Tume hiyo waliporwa magari ambayo yamewekwa Ikulu.

Aidha, Gazeti la Mtanzania la leo pia, limeandika habari, zisizokuwa za kweli vile vile, chini ya kichwa cha habari: “Bilioni 6 kuipoza Tume ya Warioba”.
Habari hiyo inamkariri mjumbe mmoja wa Tume hiyo, ambaye Gazeti halimtaji jina, akidai kuwa Tume hiyo 
inatarajiwa kupewa kiasi cha Sh. bilioni sita ikiwa ni kiinua mgongo ambako kila mjumbe atapata kiasi cha Sh. milioni mia mbili.

Habari zote mbili ni za uongo na Ikulu inapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
(a) Tume kufukuzwa kazi
Itakumbukwa kuwa moja ya mijadala mikali ya awali kuhusiana na mchakato wa Katiba Mpya ulihusu lini Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize muda wake; wengine wakitaka Tume imalize muda wake baada ya kukabidhi Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba, wengine wakitaka Tume imalize muda wake baada ya Mwenyekiti wake Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu yake Bungeni na hata wengine wakitaka wajumbe wa Tume wawe sehemu ya Bunge Maalum la Katiba.

Hatimaye, ilikubaliwa kuwa Shughuli za Tume zingefikia ukomo wake baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Kifungu hicho kinasema kuwa baada ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum chini ya Kifungu cha 20(3) (cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba) Rais, kwa Amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, atavunja Tume.

Mheshimiwa Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum la Katiba Jumanne ya Machi 18, mwaka huu, 2014 na siku iliyofuata Jumatano, Machi 19, 2014 na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais alitia saini tangazo la Serikali la Kuvunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tangazo hilo lilichapishwa katika toleo lililofuata la Gazeti la Serikali la Ijumaa, Machi 21, 2014. Gazeti la Serikali huchapishwa kila Ijumaa ya kila wiki.
Hivyo, tokea mwanzo wa mchakato mzima wa Katiba Mpya na utendaji kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapakupata kuwepo, hata wakati mmoja, shaka kuhusu siku ya Tume hiyo kumaliza kazi zake. Mwenyekiti wa Tume, wajumbe wote wa Tume, Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua fika siku ya mwisho ya Tume kukamilisha shughuli zake. Kwa mtu kujitia ameisahau siku hiyo leo ni kiwango cha juu sana cha unafiki.

Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na Ikulu haikuwa na madaraka wala mamlaka yoyote kubadilisha tarehe hiyo. Hivyo, madai ya Ikulu kuitupia virago Tume ya Mabadiliko ya Katiba hayana msingi wowote na ni jambo la kutunga tu.

(b) Muda wa kuandaa na kukabidhi nyaraka na ofisi
Hili nalo ni jambo la kutunga na kuzusha tu. Mheshimiwa Jaji Warioba alikabidhi rasmi Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Jumatatu ya Desemba 30, 2014, mbele ya wananchi viwanja vya Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Hivyo, tokea siku hiyo, Tume haikuwa tena na kazi ya kuandaa Ripoti ama Rasimu kwa sababu kazi hiyo ilikuwa imekwisha na wala isingeweza kuibadili tena Rasimu ya Katiba. Kwa maana hiyo, tokea Desemba 30, mwaka jana, kupitia miezi ya Januari, Februari mpaka Machi 18, mwaka huu, Sekretariati ilikuwa na muda wa siku 77, zaidi ya miezi unusu, kufanya maandalizi ya kukabidhi nyaraka na ofisi kwa sababu ilijua kazi yake ilikuwa inamalizika siku ambayo Mwenyekiti wa Tume hiyo angewasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum la Katiba.
Sasa katika muda wote huo, Sekretarieti ya Tume ilikuwa inafanya nini badala ya kuandaa ripoti ya makabidhiano na wakati maofisa wake walikuwa wanaendelea kulipwa mshahara na Serikali? Kwa nini walalamike hadharani leo kwa jambo ambalo lilikuwa ni la wajibu wao na wakashindwa kulifanya kwa wakati?
(c) Wajumbe wa Tume kutakiwa kurudisha magari Ikulu
Ni kweli kuwa wajumbe wa Tume walitakiwa kurudisha Ikulu magari ambayo walikuwa wanatumia kikazi kwa sababu kazi ya Tume ilikuwa imemalizika.

Pili, Tume ilijua tokea mwanzo kuwa baada ya kumaliza kazi yao, magari ambayo walikuwa wanatumia wajumbe na maofisa wa Tume hiyo yalikuwa yanatakiwa kupelekwa Dodoma kwa matumizi ya shughuli za Bunge Maalum la Katiba ambalo linakabiliwa na shida kubwa ya usafiri.

Serikali ilichukua uamuzi kuwa magari hayo yapelekwe Dodoma kwa sababu lisingekuwa jambo la busara kwa Serikali kutumia fedha za umma kununua magari mengine mapya wakati yale ya Tume bado yanafaa kufanya kazi na wala hakuna bajeti ya kufanya manunuzi ya magari mapya.

Hivyo, ni kweli magari hayo yako Ikulu, Dar es Salaam, yakisubiri kukamilika kwa taratibu za kuyapeleka Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.
(d) Wajumbe wa Tume kulipwa kiinua mgongo cha Sh. milioni 200 kila mjumbe

Hakuna shaka kuwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wamefanya kazi nzuri sana na wanastahili pongezi nyingi za wananchi. Lakini kama wanadhani kuwa Serikali ina uwezo wa kumlipa kila mjumbe kiinua mgongo cha Sh. milioni 200 basi wanajidanganya. Wala wananchi wa Tanzania hawawezi kuelewa maana kabisa ya malipo hayo makubwa kupindukia.

Alichokizungumza Rais Kikwete tokea mwanzo wa mchakato ni kwamba atafikiria kuwalipa wajumbe wa Tume aina fulani ya kifuta jasho ambacho kiwango chake atakiamua yeye na kwa wakati mwafaka na kulingana na raslimali za Serikali. Mpaka sasa hajafanya uamuzi juu ya jambo hili.

(e) Posho ya Sh. 500,000 kutwa kwa kila mjumbe wa Tume 

Ikulu pia inapenda kutoa ufafanuzi wa habari zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa wajumbe wa Tume hiyo walikuwa wanalipwa Sh. 500,000 (Laki tano) kama posho ya vikao kwa siku. Hili nalo siyo la kweli.
 


Ukweli ni kwamba wajumbe wa Tume walikuwa wanalipwa Sh. 200,000 kama posho ya vikao kwa siku. Maofisa waandamizi wa Tume hiyo walikuwa pia wanalipwa posho ya Sh. 200,000 (Laki mbili) kwa siku, maofisa wa kati walikuwa wanalipwa Sh. 150,000 kutwa na maofisa wa ngazi za chini walikuwa wanalipwa Sh. 100,000 kwa siku kulingana na taratibu za Serikali. Anayetangaza vinginevyo anajaribu tu kuwapotosha wananchi.
 

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
 

 Ikulu. Dar es Salaam.
02 Aprili, 2014

No comments: