Monday, September 14, 2015

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI AZINDUA MPANGO KABAMBE WA MJI MPYA WA KIGAMBONI

  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (Mb), akihutubia wananchi wa Kigamboni katika Uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni Katika Uwanja wa Tangamano - Mnadani Vijibweni.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mipango Miji, Bibi Immaculata Senje akitoa taarifa fupi ya Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni wakati wa Uzinduzi wa Mpango huo.
 Wasanii wa kikundi cha Ngoma za kitamaduni wakiburudisha wakati wa Uzinduzi Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni.
  Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bibi Sophia Mjema akizungumza na wananchi wa Kigamboni katika Uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni, kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bwn. Alphayo Kidata.
 Aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni Faustine Ndugulile akizungumza na wananchi wa Kigamboni katika Uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni, nyuma yake ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,William Lukuvi (Mb), Katibu Mkuu Bwn. Alphayo Kidata na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bibi Sophia Mjema.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (Mb) akikata utepe kuzindua Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni, kulia ni Naibu wake Bibi Angela Kairuki (Mb), wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bibi Sophia Mjema na aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni Faustine Ndugulile.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Mb) akionesha vitabu vya Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni.
 Wananchi mbalimbali ambao ni wakazi wa Mji wa Kigamboni wakisilikiza maelezo mbalimbali kutoka kwa viongozi katika mkutano wa hadhara wakati wa Uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni.
Picha za Mji Mpya wa Kigamboni.
HOTUBA YA MGENI RASMI, WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, MHE. WILLIAM V. LUKUVI, KATIKA UZINDUZI WA MPANGO KABAMBE WA MJI MPYA WA KIGAMBONI TAREHE 12 SEPTEMBA 2015 KATIKA UWANJA WA
TANGAMANO – MNADANI VIJIBWENI
 

Mhe. Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mhe. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Temeke,
Makatibu Wakuu,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana

Ndugu Wananchi,
Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Serikali kuwashukuru wananchi wa Kigamboni kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mkutano huu wa uzinduzi wa Mpango Kabambe “Master Plan” wa Mji Mpya Kigamboni ambao tumeusubiri kwa muda mrefu.

Ndugu Wananchi,
Kama nilivyowahi kuwaeleza siku za nyuma dhana ya Mji Mpya wa Kigamboni iliasisiwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya kuingia madarakani. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alitoa agizo hilo  kwa Wizara mwaka 2006   na baadaye kuingizwa kwenye  Ilani ya CCM  ya mwaka 2010-2015 ambayo ilikusudia kuinua hadhi  ya Jiji  la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla katika kuleta ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii. Agizo hilo limetekelezwa kwa kuandaa Mpango Kabambe wa Mji Mpya Kigamboni ambao umezingatia hatua muhimu kwa mujibu wa sheria na mahitaji ya wadau.

Ndugu Wananchi,
Matokeo yanayotarajiwa katika utekelezaji wa mpango ni pamoja na:
i.         Kuwa na maeneo ya uwekezaji yatakayotoa fursa za ajira  kwa wananchi na kuleta ustawi wa kiuchumi na kijamii na hivyo kuwezesha kupanda kwa viwango vya uchumi kwa mtu mmoja moja na Taifa kwa ujumla;
ii.         Kuwa na mji uliopangwa vizuri  na wenye mazingira mazuri yanayokidhiviwango vya usalama vya kimataifa hivyo  kutoa fursa kwa wazawa na wageni kutoka nje ya nchi kuishi kwa amani na utulivu;
iii.         Kuwa na mji wenye mfumo  wa kisasa wa njia za mawasiliano na miundombinu ya kuiunganisha nchi yetu na mataifa mengine kiutandawazi na hivyo kumudu ushindani wa kimataifa katika  masuala ya kiutandawazi;
iv.         Kuwa na mji wenye huduma za kisasa za ofisi, na kumbi za  mikutano, maeneo ya biashara, hoteli za kitalii zenye fukwe nzuri katika hadhi ya  kimataifa;
v.         Kuwa na mji uliojengwa kwa viwango vya kimataifa vinavyozingatia mazingira safi, miundombinu inayoendana na shughuli za kiuchumi hivyo kuimarisha afya za wananchi.

Ndugu Wananchi,
Zimekuwepo jitihada  mbalimbali zilizofanywa na serikali kwa kushirikiana na ninyi wananchi na wadau wengine katika  uandaaji wa Mpango huu. Naomba nitumie fursa hii kuwashukuru  wananchi wa Kigamboni na wadau walioshiriki  kwa namna mbalimbali katika kufanikisha ukamilishaji wa Mpango huu. Baadhi yenu mlitoa maoni na mapendekezo kuhusu Mpango, kupitia na kuboresha nyaraka mbalimbali zilizohusiana na Mpango na kuzihuisha kwa lengo la kuboresha na kuukamilisha Mpango kwa maslahi ya umma.

Mojawapo ya masuala yaliyoshughulikiwa ni pamoja na kupunguza eneo la  Mpango kutoka  hekta  50,934  hadi  6,494,   kutoka Kata tisa (9) na kubaki sita (6). Kurekebisha matangazo ya zamani na kutayarisha matangazo mapya  ambayo ni Namba 257, 258 ya tarehe 17/7/2015 na Tangazo Namba 301 la tarehe 24/7/2015.  Mchakato  huu ulifuata misingi ya utawala bora kwa njia ya ushiriki na ushirikishwaji wa wadau wote.

Ndugu wananchi,
Kwa mujibu wa dhana mpya, uendelezaji wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni utafanyika kwa namna kuu tatu:
       i.            Wamiliki wa ardhí kuendeleza maeneo yao kulingana na Mpango;
    ii.            Wamiliki wa ardhí kuingia ubia na waendelezaji wengine na kuendeleza maeneo yao kulingana na Mpango; na,
 iii.            Wamiliki wa ardhí kuuza ardhí yao kwa bei ya soko na wanunuzi kuiendeleza kulingana na Mpango.

Maeneo yote yanayopitiwa na miundombinu na huduma za kijamii yatatwaliwa na Serikali na wananchi kulipwa fidia stahili kwa mujibu wa Sheria za nchi.

Ndugu Wananchi,
Hatua iliyopo mbele yetu sasa ni kuutekeleza Mpango kwa kuanza na shughuli zifuatazo: kutambua na kupima maeneo ya miundombinu  tukianza na miundombinu ya barabara kubwa zenye viwango vya upana wa mita 70 na 140 zilizopo kwenye eneo la Mpango; Kufanya uthamini wa maeneo yanayopitiwa na barabara na kuaadaa mipango ya kina. Zoezi hili litaanza rasmi leo mara baada ya uzinduzi wa Mpango. Wale wote watakaopitiwa na miundo mbinu ya barabara, watalipwa vizuri kwanza kabla ya ujenzi wa miundo mbinu yenyewe.  Kwa hiyo ni marufuku kwa mtu kuondolewa na kuvunjiwa nyumba yake bila kulipwa fidia stahiki.

Nichukue fursa hii tena kuwashukuru kwa namna ya pekee wananchi wa Kigamboni kwa uvumilivu wenu na ushiriki wenu uliotuwezesha kwa pamoja kufikia hatu hii ya leo; ambayo imetuwezesha kuandika historia kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Baada ya kusema hayo natamka kuwa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni umezinduliwa rasmi leo tarehe 12 Septemba, 2015.

KARIBUNI  SANA!

RISALA FUPI YA UZINDUZI WA MPANGO KABAMBE WA
MJI MPYA WA KIGAMBONI


Mhe.  Mgeni Rasmi,
Awali ya yote tunapenda kukushukru kwa kukubali kutoa muda wako na kuja katika tukio hili muhimu la kihistoria tukizingatia kwamba unayo majukumu mengi ya kitaifa yanayokukabili.

Mhe. Mgeni Rasmi,
Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni ulianza kuandaliwa mwaka 2008 baada ya kusudio la kuandaa Mpango kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 229 la tarehe 18/10/2008.

Mhe. Mgeni Rasmi,
Mchakato wa Uandaaji wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni ulipitia hatua mbalimbali kulingana na Sheria ya Mipangomiji Na. 8 ya mwaka 2007. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na  kufanya uhamasishaji wa wadau mbalimbali na kutoa elimu kupitia warsha na mikutano.

Mhe. Mgeni Rasmi,

Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni umeainisha matumizi mbalimbali ya ardhi katika Kanda kuu tano (5)
Kanda hizo ni:
(i)              Eneo la Kitovu cha Mji (CBD) ambalo ni maalum kwa shughuli za  biashara
(ii)           Eneo la Makazi
(iii)        Eneo la Viwanda na Utafiti
(iv)         Maeneo ya Taasisi zikiwemo za elimu
(v)            Eneo la Utalii na Burudani.

 Maeneo haya yote yanaunganishwa na mitandao ya Barabara, Reli na usafiri wa majini.

Mhe. Mgeni Rasmi,
Hatua iliyofikiwa leo katika utekelezaji wa Mpango wa Uendelezaji Mji Mpya wa Kigamboni ni mafanikio makubwa yaliyotokana na juhudi zako katika kuhakikisha kwamba wanakigamboni wananufaika na mpango huu. Ushirikiano wa wadau mbalimbali hususan wananchi wa Kigamboni kupitia wawakilishi wao umechangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia ukamilishaji wa maandalizi ya Mpango huu.

Mhe. Mgeni Rasmi,
Uzinduzi wa Mpango huu ni mwanzo wa utekelezaji wake kwa kuanzia na ufunguzi wa barabara kuu zenye upana wa mita 140 na mita 70. Ufunguaji wa barabara hizi kuu utasaidia kutambua maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya mbalimbali ya ardhi kama yalivyoainishwa hapo juu. Kabla ya kuanza kwa upimaji wa barabara hizi kuu wananchi wanaopitiwa na miundombinu hii watatambuliwa, kufanyiwa uthamini wa mali zao na kulipwa fidia stahiki.

Kazi nyingine inayotarajiwa kuanza mara tu baada ya uzinduzi huu ni utayarishaji wa mipango ya kina ambapo baada ya kuidhinishwa itawezesha upimaji wa maeneo mengine yaliyotengwa kwa matumizi mbalimbali. Hii itawapa fursa wananchi kuanza kuendeleza maeneo yao kulingana na mpango.
 
Hitimisho
Mhe. Mgeni Rasmi,
Naomba kuhitimisha kwa kusema kwamba tukio la leo linafungua ukurasa mpya katika uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni.

Tunakushukuru sana.

No comments: