Tuesday, September 23, 2014

SERIKALI IMEWATAKA WANANCHI KUJIHADHARI NA VISHOKA KATIKA UPIMAJI ARDHI

01Mkurugenzi Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mikazi Bw. Justo Lyamuya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taratibu za upimaji wa viwanja nchini na kutoa tahadhari kwa wananchi kutumia makampuni ambayo hayakusajiliwa katika shughuli za upimaji Ardhi, wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Katibu wa Baraza la Upimaji na Uthamini wa Wizara Hiyo Bw. Nassor Duduma.
02Katibu wa Baraza la Upimaji na Uthamini wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mikazi Bw. Nassor Duduma akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu ufuataji wa Sheria katika shughuli za upimaji ardhi kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1957 sura namba 324, wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Afisa Habari wa Wizara Hiyo Bw. Clarence Nanyaro.
Frank Mvungi-Maelezo
Serikali imewataka wananchi kujihadhari na makampuni yanayojiingiza katika kazi za upimaji ardhi au uthamini bila ya kusajiliwa  na bodi au Halmashauri zenye mamlaka ya kusimamia taaluma husika.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi bw.Justo Lyamuya wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga kutoa utaratibu unaotakiwa kufuatwa na wananchi katika upimaji ardhi.
“Hadi sasa wapima ardhi waliosajiliwa ni 290 wakati makampuni yaliyosajiliwa na Baraza la Taifa la wapima na wathamini ardhi ni 58” hivyo hakuna haja ya wananchi kutapeliwa na vishoka. Alisema Bw. Lyamuya.
Akifafanua Lyamuya amesema kuwa ni vyema wananchi wakatumia makampuni yaliyosajiliwa kufanya kazi ya kupima ardhi ili kuepuka migogoro ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na ukiukwakwaji wa sheria na taratibu za upimaji ardhi.
Akifafanua kuhusu wathamini (valuers) Lyamuya amesema hadi sasa wataalamu waliosajiliwa ni 320 na makampuni yalisajiliwa na Baraza ni 54.
Pia Lyamuya alisema kuwa kazi za upimaji viwanja zitakazowasilishwa Wizarani ambazo hazikufuata taratibu na kwa mujibu wa sheria ya upimaji Ardhi sura 324 ya mwaka 1957 hazitapokelewa.
Pia mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika upimaji wa ardhi (mashamba na viwanja) lyamuya amesema upimaji usiozingatia ushirikishwaji na kutambua mipaka kwa maridhiano hautapokelewa.
Aidha makampuni ya upimaji yanayowasilisha kazi za upimaji kwa Mkurugenzi waUpimaji na Ramani ambazo hawakuzisimamia wao wenyewe au wawakilishi wao na kudhibitika;kazi hizo hazitapokelewa na kwa mujibu wa sheria za kusajili makampuni ya upimaji Na.2 ya mwaka 1977 yataadhibiwa ikiwa ni pamoja na kusimamishwa.
Halmashuri ya Taifa ya wapima Ardhi ni chombo cha Serikali kilichoundwa kwa mujibu wa sheria Na.2 ya mwaka 1977,Jukumu kubwa la chombo hiki ni kufanya usajili wa wataalam wapima Ardhi,kusimamia weledi wa taaluma na mwenendo wa utendaji katika masuala ya kupima ardhi (Land Survey) kuthamini mali (property valuation) na kuendeleza ardhi (estate management).

No comments: