Wafanyabiashara Namanga walalamikia kunyanyaswa nchini Kenya

Wafanyabiashara wa Namanga na Wilaya ya Longido wameiomba Serikali iwajengee Soko kubwa Namanga ili waepukane na usumbufu wanaoupata wanapokwenda Kenya kuuza mifugo, mazao na bidhaa nyingine.

Wafanyabiashara hao walitoa ombi lao jana Septemba 19 wakati wa mkutano na Maofisa wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki wanaotembelea mipaka mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya Mtangamano wa Afrika Mashariki.

Baadhi ya manyanyaso wanayopata wanadai ni kuombwa kitu kidogo, kupewa malipo kidogo ya bidhaa zao kuliko bei ya soko na kusumbuliwa kuhusu ubora wa bidhaa wakati bidhaa zao zimetimiza viwango vyote.

Uongozi wa Wilaya ya Longido umetenga eneo la heka 120 kwa ajili ya soko ili wafugaji na wakulimna wauzie bidhaa zao hapo.

Hiyo pia itasaidia Wanunuzi kutoka Kenya waje kununua sokoni hapo na hivyo wakulima na wafanyabishara wa Tanzania kupata bei nzuri na kuepuka usumbufu wanaoupata sasa. 

Wafanyabishara hao pia wamesema ujenzi wa soko utasaidia kuzuia Wakenya kwenda mashambani na kununua mazao moja kwa moja kwa wakulima.

Akizungumza na wafanyabiashara hao Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Graceana Shirima alisema Serikali itashugulikia haraka malalamiko yao ikiwa pamoja kuharakisha ujenzi wa masoko mipakani.

Shirima, ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Joyce Mapunjo, alishauri uongozi wa Wilaya ya Longido kuanza na utaratibu wa gulio wakati wakiendelea na mikakati ya ujenzi wa soko.

Mweka Hazina wa Wilaya Issai Mbiru alisema tayari Wilaya imepata fedha Shilingi bilioni 2.3 kutoka kwa wafandhili na ujenzi wa soko hilo utaanza muda si mrefu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara Bi. Graceana Shirima (kulia) akimkabidhi machapisho mbalimbali Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido Bw. Dunford Peter wakati wa ziara ya kuonana na wafanyabiashara wa Namanga tar. 19-9-2014
Malori yakisubiri kukamilisha taratibu za kuvuka Mpaka wa Namanga kuingia Tanzania kwa kutumia utaratibu wa zamani. Ujenzi wa OSBP utarahisisha Malori na wasafiri kupita.
Jengo la Utoaji wa Huduma za Pamoja Mpakani (OSBP) Namanga (upande wa nyuma) likiwa katika hatua za mwisho kukamilika. OSBP inatarajiwa kupunguza urasimu wa kuvuka mipakani.
Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Ufuatiliaji na Tathmini (katikati) akisikiliza malalamiko ya wafanyabiashara wa Namanga tar. 19-9-2014. kushoto ni Mchumi Othman Chanzi na kulia ni Katibu Tawala, Longido Dunford Peter.
Baadhi ya Wafanyabiashara wa Namanga na Longido wakiwa katika mkutano wa pamoja na Wizara kuhusu kufuatilia kero wanazopata mipakani. Mkutano huo ulifanyika tarehe 19-9-2014. Wengine ni wawakilishi wa SIDO, TAHA na TCCIA Mkoa wa Arusha.

Comments