RAI imetolewa kwa vyombo vya habari, taasis mbalimbali, vikundi vya kijamii, wananchi na serikali kushirikiana kwa pamoja katika kujenga jamii yenye maadili kuanzia ngazi ya familia ili kuleta maendeleo katika nchi.
Hayo yamebainishwa na Afisa kutoka IQ Management Solutions Joel Nanamka wa wakati akizungumza na gazeti hili jana jiji Dar es Salaam.
Alisema iwapo kutakuwepo kwa ushirikiano baina ya sekta hizo ni wazi kuwa jamii itazingatia maadili katika suala lolote ambalo linafanyika kwa maslahi ya Taifa.
Nanamka alisema vyombo vya habari kama moja ya muhimili usio rasmi bado havijafanya kazi ya dhati ili kuweza kuibadilisha jamii ambayo inaonyesha dhahiri kupotea katika misingi ya utu.
Afisa huyo alisema ukosefu wa maadili hasa katika sekta mbalimbali za serikali kumekuwa kukichangia ukosefu wa huduma bora na zenye viwango kwa jamii.
“Kimsingi suala la kuwepo kwamaadili ni mtambuka ila kwa mtazamo wetu katika tafiti mbalimbali tunaona kuwa nafasi ya vyombo vya habari katika kufanikisha hilo ni kubwa hivyo vinapaswa kubadilika kutokana na ukweli kuwa watu wengi wanafikiwa”, alisema.
Alisema IQ Management Solutions imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha kuwa maadili yanakuwepo kwa kanuni, sheria, zawadi na matisha pamoja na adhabu ambazo zitakuwa katika mtazamo hasi.
Kwa upande wake Afisa Programu kutoka taasisi ya Afrika Leadership Initiative Foundation Limited Alice Mwiru alisema katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo kwa jamii yenye maadili taasisi yao imejikita kufanya kazi na vijana ambao wanaonyesha nia za kuongoza.
Mwiru alisema wao wanaamini kuwa kuwepo kwa viongozi wenye maadili ni chachu ya kuwepo kwa jamii ambayo itakuwa katika misingi hiyo.
“Sisi ALI EAF tunaamini kuwa jamii ikikuwa kwa misingi ya maadili hasa kuanzia utotoni ni wazi kuwa kila Mtanzania atakuwa kwenye misingi hiyo kwa faida yake na nchi kwa ujumla”, alisema
Comments