UKOSEFU WA UELEWA NA IMANI POTOFU NI MOJA YA CHANZO CHA UNYANYAPAAJI KWA WATOTO WENYE USONJI

img_0858Na Anna Nkinda – Maelezo, New York
24/9/2014 Ukosefu wa uelewa na imani potofu miongoni mwa wanajamii ni moja ya chanzo cha unyanyapaa kwa watoto wenye tatizo la usonji (Autism) .
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Mama Salma Kikwete wakati akiongea na Prof. Andy Shih ambaye ni Makamu wa Rais mwandamizi wa Mambo ya kisayansi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Autism Speaks yenye makao yake mjini New York.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema jamii bado haina uelewa kuhusu tatizo la usonji kwani kuna baadhi ya watu wanahusisha tatizo hilo na mambo ya ushirikina lakini kama jamii itakuwa na uelewa tatizo la unyanyapaa litapungua au kwisha kabisa.
Alisema usonji bado ni tatizo nchini Tanzania na nchi zingine lakini wazazi wengi wanaona aibu kusema hadharani wana  watoto wenye matatizo hayo na hivyo kuwa vigumu kwa watoto hao kupata huduma muhimu ikiwemo elimu.
“Tunatakiwa kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu waliobobea katika taaluma hii ili kuhakikisha  jamii inakuwa na uelewa kuhusu tatizo hilo kwa kufanya hivyo watoto hawa watapata huduma za muhimu kama elimu na afya”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Prof. Shih alisema Taasisi yake iko tayari kufanya kazi na WAMA ili kuwasaidia watoto wenye tatizo la usonji ili waweze kupata elimu na huduma ya afya kama watoto wengine.
Prof. Shih alisema tatizo la unyanyapaa bado ni kubwa kwa watoto lakini kama jamii itapata elimu na kulifahamu tatizo hilo itaweza kuwasaidia watu wenye matatizo hayo na hivyo kupunguza tatizo la unyanyapaa.
Usonji ni hali ya udhaifu katika ukuaji wa ubongo ambayo huleta athari kubwa katika mawasiliano, mahusiano ya kijamii na utambuzi.Tatizo hili ni la dunia nzima na bado hakuna maelekezo kamili ya chanzo chake wala tiba.
Wanaoathirika zaidi ni watoto wa kiume kuliko wa kike kwa uwiano wa nne kwa moja hii ikiwa na maana kuwa kila watoto watano wenye usonji wanne ni wa kiume na mmoja wa kike.
Mwaka 1997 wizara ya Elimu na Utamaduni ikishirikiana na wanachama wa National Association for People with Autism in Tanzania (NAP-T) walianzisha kitengo cha watoto wenye usonji katika shule ya msingi Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha kutoa huduma.
Hivi sasa Serikali inavitengo vitano, viwili vipo Dar es Salaam, viwili Arusha na kimoja Morogoro. Pia kuna vitengo kadhaa vilivyoendeshwa na watu binafsi.

Comments