BUNGE MAALUM LA KATIBA LAPENDEKEZA MAKAMU WATATU WA RAIS

CHENGE2Bunge Maalum la Katiba limependekeza muundo wa uongozi wa Serikali utakuwa na  Makamu watatu wa Rais wa Jamhuri Muungano  wa Tanzania.
 Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mwenyekiti wa  Kamati ya Uandishi wa Bunge Maalum la Katiba,Mhe. Andrew Chenge wakati akiwasilisha  Rasimu ya Katiba inayopendekezwa  wakati wa kikao cha arobaini na mbili cha Bunge hilo.
 Amesema kuwa katika mapendekezo hayo mgombea mwenza ndio atabaki kuwa  Makamu wa Kwanza wa Rais, na kwa upande wa Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Pili na Waziri Mkuu atakuwa Makamu wa tatu wa Rais.
 Amesema kuwa Kamati hiyo ya uandishi imeona ni busara mgombea mwenza kuendelea kuwa Makamu wa Rais kwa kuwa  itakuwa rahisi kwake kukaimu uongozi kama itatokea bahati mbaya Rais aliyemadarakani  hatakuwepo kwa namna moja au nyingine kwani ataendeleza ilani za mwenzake kuliko atakavyokuwa wa kutoka Zanzibar kama kutakuwa na vyama viwili tofauti vinatawala.
 Kwa upande wa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa pili , Chenge amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha muungano kwani kiongozi huyo ni kiungo muhimu katika kudumisha Muungano.
 “Suala  la Rais wa Zanzibar kuwa Makamu ni la msingi kwa kuwa ni kiungo muhimu ikizingatia historia ya nchi tangu mwaka 1964 muungano ulipoasisiwa ilikuwa hivyo hadi mfumo wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1992,” alisema Mhe. Chenge huku akiongeza kuwa anakuwa hivyo kwa nafasi yake.
 Ameongeza kuwa Waziri Mkuu anakuwa Makamu wa Tatu kwa mujibu wa Cheo chake. 

Comments