Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali wa ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Gabriel Madebe akifungua semina ya wadau ya uhamasishaji wa matumizi takwimu za kilimo zinazopatikana kupitia Kanzi rasmi ya takwimu za kilimo inayopatikana katika anwani ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya www.nbs.go.tz jana jijini Dar es salaam.Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Bi. Julia Stone akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa semina ya uhamasishaji wa matumizi ya Kanzi ya takwimu za Kilimo nchini jana jijini Dar es salaam.Mratibu wa Kanza ya Takwimu za Kilimo Tanzania Bw. Basike Mteleka akijibu maswali ya wadau mbalimbali waliohudhuria semina ya uhamasishaji wa matumizi ya Kanzi ya takwimu za Kilimo nchini .
Wadau mbalimbali waliohudhuria semina ya uhamasishaji wa matumizi ya Kanzi ya takwimu za Kilimo nchini Tanzania wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa semina hiyo jana jijini Dar es salaam.
NBS YASISITIZA MATUMIZI YA KANZA (DATA BASE) YA TAKWIMU ZA KILIMO
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
26/9/2014, Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imewataka watunga Sera, taasisi, mashirika, na wadau mbalimbali wa maendeleo kuitumia Kanza (Data base) rasmi ya takwimu za Chakula na Kilimo iliyoanzishwa hapa nchini kwa lengo la kutoa takwimu za Kilimo kutoka katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakati wa ufunguzi wa semina ya kuhamasisha matumizi ya Kanza hiyo leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu wa ofisi hiyo Bw. Gabriel Madembwe amesema upatikanaji wa taarifa za sekta ya Kilimo na Chakula kutoka katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji hapa nchini umerahisishwa kupitia Kanzi hiyo inayopatikana kupitia tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya www.nbs.go.tz
Amesema takwimu zilizo katika Kanza hiyo zitaiwezesha serikali, watunga sera na wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya kilimo nchini.
Amesema matumizi ya Kanza hiyo yanawarahisishia wadau hao kupata taarifa za Kilimo na chakula kwa urahisi zilizokusanywa kutoka katika taasisi mbalimbali na wizara zinazohusika na sekta ya Kilimo hapa nchini.
Amesema matumizi Kanza yataondoa hali iliyokuwepo hapo awali ya ugumu wa upatikanaji wa takwimu kutokana na mtawanyiko wa takwimu hizo na kuwataka wadau wote wa sekta hiyo walio katika ngazi ya maamuzi kuielewa na kutumia.
Amefafanua kuwa takwimu zinazowekwa katika Kanza hiyo zinahusu Kilimo, Uvuvi, Biashara, Uzalishaji na upatikanaji wa chakula katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na kuongeza kuwa kazi ya uwekaji na uhuishaji wa takwimu hizo inafanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa ushirikiano wa wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Oswald Luboha akitoa ufafanuzi kuhusu Kanzi hiyo amesema ilianzishwa mwaka 2005 na kuzinduliwa rasmi mwaka 2012 kwa lengo la kuweka pamoja takwimu za kilimo ili wadau wa sekta ya Kilimo waweze kuzipata kwa urahisi.
Amesema Tanzania ina maeneo mengi yanayofaa kwa uzalishaji kwa shughuli za kilimo hivyo kuna umuhimu wa maeneo hayo kujulikana, ukubwa wake na mazao yanayolimwa katika maeneo hayo
Amesema Tanzania inafanya vizuri kwa kufanya sensa ya Kilimo kila baada ya miaka 5 ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika ya Mashariki hivyo kupunguza muda wa kufanya sensa ya kilimo kutoka miaka 10 iliyoainishwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Naye mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Bi. Julia Stone akizungumza katika semina hiyo ya uhamasishaji amesema kuwa Tanzania inafanya vizuri katika kuhakikisha kuwa takwimu sahihi za kilimo zinapatikana kutokana na ushirikiano uliopo wa wizara husika na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Kuhusu mchango wa FAO katika kufanikisha tafiti mbalimbali zinazoendelea hapa nchini amesema Tanzania itaendelea kunufaika kutokana na kuwa miongoni mwa nchi 17 za Afrika zinazoshirikiana na Shirika la Chakula Duniani (FAO) kupitia taasisi ya Bill na Melinda Gates.
Comments