Baadhi ya Kamati za Bunge Maalum la Katiba zimependekezwa kuwepo kwa Ibara mpya inayohusu kuanzishwa kwa Tume za Huduma za Sekta, mbalimbali ikiwemo ya Afya, Elimu , Walimu na nyinginezo ili kuweza kukabiliana na matatizo yanayowakumba.
Kamati hizo zimependekeza suala hilo, katika sura ya 13 na 14 ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Hayo yamebainika leo wakati wa uwasilishaji wa taarifa za Kamati Namba Moja hadi Kamati Namba Kumi na Mbili za Bunge hilo kuhusu uhakiki wa Rasimu hiyo uliofanyika kwenye kikao cha arobaini na tatu kilichofanyika mjini Dodoma.
Taarifa hizo,ambazo zimewasilishwa na baadhi ya wenyeviti wa Kamati hizo na baadhi ya wajumbe kutoka 201 waliopewa ridhaa za kuwasilisha.
Baadhi ya Kamati za Bunge hilo,ambazo zimependekeza suala ni Kamati namba 5 na 6.
Akizungumzia kuhusu suala hilo, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita ya Bunge hilo, mjumbe wa Bunge hilo, Charles Mwaijage alisema Kamati yake inapendekeza kuongeza Ibara mpya ya 208A mara baada ya Ibara ya 208 itakayosomeka kama ifuatavyo:
“Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta za huduma za jamii kwa wananchi, Bunge litatunga sheria ya kuanzisha Tume za Huduma za Sekta hizo, kwa ajili ya uendeshaji wa ufanisi zikiwemo za Elimu,Afya na nyingine kadri mahitaji yatakavyojitokeza ,” alisema Mwaijage.
Kwa upande wa Kamati Namba Tano ya Bunge Maalum la Katiba,mjumbe wa Bunge hilo, Paul Makonda akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti alisema, Kamati hiyo inapendekeza katika sura ya 14 kuongezwa kwa kifungu kipya kitakachounda Tume ya Utumishi wa Walimu na kusomeka :
(1)Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Walimu itakayoshughulikia, mishahara, maslahi, ajira na masuala ya kinidhamu kwa walimu.
(2)Bunge litatunga sheria itakayoweka masharti kuhusu muundo, majukumu mambo mengine kuhusu utkelezaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu.
Akizungumzia kuhusu suala hilo, Ezekiah Olouch, aliomba Kamati ya Uandishi ya Mhe. Andrew Chenge kuliangalia.
Alisema zawadi ambayo watamkumbuka na walimu, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Samuel Sitta na Bunge hilo kwa walimu hao ni kuingizwa kwa tume hiyo ambayo itasaidia kutatua mattaizo ya walimu kwa asilimia 90.
Comments