Thursday, June 11, 2015

KITUO CHA DHARURA CHA KUPOKEA NA KUTOA TAARIFA ZA MAJANGA YA MABADILIKO YA TABIANCHI KUANZISHWA

01
Mratibu mradi kitaifa wa Kuimarisha mfumo wa habari za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari ya mapema nchini, Alfei Daniel akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya utekelezaji wa mradi huo kwa wajumbe wa  kamati ya Maafa Wilayani Arumeru mkoani Arusha, (hawapo pichani), tarehe 10 Juni, 2015, kulia kwake ni mwezeshaji wa mafunzo hayo  kutoka  Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Dkt Silvia Materu  na  mwezeshaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania , Bwire Kahitila.
02
Washiriki wa mafunzo ya utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha mfumo wa habari za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari ya mapema nchini, kutoka kamati ya maafa wilayani Arumeru,  mkoani Arusha  wakifuatilia mafunzo hayo tarehe 10 Juni, 2015, wa kwanza ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Usa river, SP. Msolo Msolo.
03
Washiriki wa mafunzo ya utekelezaji mradi wa Kuimarisha mfumo wa habari za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari ya mapema nchini, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Danstan Mallya (mwenye tai) mara baada ya kufungua mafunzo hayo wilayani Arumeru,  mkoani Arusha  tarehe 10 Juni, 2015.
………………………………………………………..
Na. Mwandishi Maalum
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu Maafa kupitia mradi wa kuimarisha mifumo ya habari za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari nchini, itaanzisha kituo cha dharura ambacho kitafanya kazi masaa 24 kwa ajili ya Kuimarisha upatikanaji wa taarifa za Hali ya hewa, mabadiliko na viashiria vya mabadiliko ya tabia nchi ili kutengeneza mifumo imara ya Tahadhari na utaratibu wa kuhimili majanga yanayotokana na mabadiliko hayo . 
Kituo hicho kitakuwa na mfumo na utaratibu maalum wa mawasiliano wa kutoa taarifa za viashiria vya athari za mabadiliko ya tabia nchi kupitia asasi za serikali na taasisi zisizo za kiserikali. Aidha, kituo hicho kitakuwa na jukwaa la upashaji wa habari za hali ya hewa ambapo wananchi kupitia simu zao za mikononi, au vifaa maalum vitakavyowekwa katika maeneo wanayoishi, wataweza kupokea taarifa za hali ya hewa za wakati huo huo na majanga yanayowezekana kutokea katika eneo lao.
Akiongea wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Maafa Wilayani Arumeru, Mratibu Mradi huo Kitaifa, Alfei Daniel, alisema tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imeshakamilisha upembuzi yakinifu wa uanzishaji wa kituo hicho kwa kuanisha idadi ya watumishi, eneo linalofaa kituo hicho kujengwa pamoja na masuala ya kifedha.
“Kituo hiki kitakuwa endelevu hata mradi huu ukimalizika utekelezaji wake, kwani mradi una lengo la kuleta maendeleo chanya ya hali ya hewa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili Wananchi kuwa na uwezo wa kupata taarifa sahihi za mapema zinazoonesha athari zitakazojitokeza ili kuandaa mikakati ya kukabiliana na hatari hizo” alisisitiza Alfei. 
Alfei aliongeza kuwa tayari mradi huo umeshaanza kuimarisha uwezo wa TMA na Mabonde ya Maji ya Pangani na Ruvuma kwa kuboresha miundo mbinu ya upatikanaji wa takwimu za hali ya hewa kwa muda mfupi na kwa ajili ya kupata taarifa za mapema kuhusu mafuriko na ukame. 
Akiongea wakati wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Danstan Mallya, alibainisha kuwa kituo hicho kikianzishwa kitaongeza uelewa mkubwa kuhusu taarifa za hali ya hewa, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uwezo wa kutambua yanayoweza kutokea kwenye maeneo yao hali hii itasaidia jamii husika sana taarifa kujiinua uchumi wao.
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya maafa zilisaini mkataba wa kutekeleza mradi huo tangu mwaka 2014 ikiwa watekelezaji ni Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Ofisi za Bonde la Pangani, Ofisi za Bonde la Ruvuma, Halmashauri ya wilaya ya Meru, Mkoani Arusha na Halmashauri ya wilaya ya Liwale, mkoani Lindi .

No comments:

KIPANGULA: WAHITIMU WA HABARI WATAFAIDIKA NA MABORESHO YA KANUNI

  Na Mwandishi Wetu Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amewashauri Waandishi ...