Tuesday, June 23, 2015

UHAKIKI WA VIKUNDI VYA VIJANA KATIKA MKOA WA LINDI NA MTWARA WAFANYIKA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Bw. Nicholous Kombe akimsikiliza Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya akimshukuru kwa Halmashauri hiyo kusaidia kikundi cha vijana kwa kuwawezesha fedha na udongo kwa ajili ya kutengeneza matofaliya kufungamana. Katikati ni Meneja wa NHC Mkoa wa Lindi Bw. Mussa Patrick Kamendu.

Kikundi cha vijana cha Ruangwa Materials Group katika Halmashauri ya Wilaya Ruangwa kimeshatengeneza matrofali kwa kutumia mashine ya msaada kutoka NHC. Halmashauri ya Wilaya hiyo imeamua kuyatumia matofali ya vijana hawa kujengea zahanati na majengo mengine yanayohitajika katika Halmashauri zikiwemo nyumba za Waalimu.

Jengo la Ofisi ya kikundi cha vijana cha Narunye(hakuna kutegeana) katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini likiwa limeonwa na Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kama inavyoonekana. Kikundi hiki kimeshaanza kupata maombi mengi ya matofali kutoka kwa wananchi wanaohitaji.
Meneja wa NHC Mkoa wa Lindi Bw. Mussa Patrick Kamendu akitoa mawaidha kwa kikundi cha vijana cha Narunye  kilichopo katika Wilaya ya Lindi vijijini baada ya kutembelea kikundi hicho kukagua kazi zake.Vijana hawa wanajihusisha pia na utunzaji mazingira.
Baada ya Wakurugezi wa Halmashauri za Kilwa na Lindi Vijijini kutokuwa karibu na vikundi vya vijana, Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC na Meneja wa Mkoa wa Lindi waliweza kufanya  mazungumzo  nao ya kina na hatimaye wamekubali kuwasaidia vijana waliopewa msaada wa mashine na NHC katika Halmashauri zao ili waweze kujiajiri. Kulia ni Bi.  Oliver Vavunge ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini na wa pili kulia  ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilwa Bi. Maimuna  Mtanda.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi  Bw. Daniel Kaluse hakuwa nyuma kutembelea kikundi cha Vijana na Maendeleo kilichopo eneo la Mitwero nje kidogo ya Manispaa hiyo ili kuwapa moyo na kufahamu maendeleo yao akiwa ameandamana na ujumbe  wa NHC. 
  
Meneja wa NHC Mkoa wa Mtwara Bw. Joseph John akitoa taarifa ya Mkoa kwa Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC ya maendeleo ya vikundi vya vijana waliosaidiwa mashine na NHC . Katika taarifa yake Meneja huyo alisikitishwa na vijana wa Mkoa wa Mtwara kushindwa kutumia kikamilifu msaada huo na akalaumu Halmashauri za Mkoa huo kushindwa kushiriki kikamilifu katika programu hiyo ya kusaidia vijana.
Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya akikemea na hatimaye kukinyanganya mashine kikundi cha Likonde katika Manispaa ya Mtwara kwa kuifungia stoo mashine waliyopewa msaada na NHC  bila kufanya kazi iliyokusudiwa ya kufyatua matofali. Mashine hiyo itapewa kikundi kingine ili itumike kikamilifu.

Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya akiwa Wilayani Tandahimba akikagua matofali yaliyotengenezwa na kikundi cha vijana cha Maendeleo Group kilichopewa msaada wa mashine  na NHC. Kikundi hiki kinasubiri kulipwa na Halmashauri matofali hayo yanayotarajiwa kujengea nyumba za waalimu. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tandahimba Bw Dennis Mwaitete akielezea mkakati wa Halmashauri yake wa kusaidia vijana ulivyo alipotembelewa na ujumbe wa NHC uliokuwa ukihakiki vikundi vya vijana Mkoani Mtwara.

Kikundi cha vijana cha Umoja Lekanelo kilichopo Wilaya ya Newala  kilichoshindwa kutumia kikamilifu mashine ya msaada kilichopewa na NHC kiliweza kupokonywa mashine hiyo jana. Wilaya ya Newala ina shughuli za madini na kilimo cha korosho kiasi cha kuwafanya vijana kushindwa kujihusisha kikamilifu na mradi wa kufyatua matofali.
Mkurugenzi  Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Marx Kamaoni akizungumza na ujumbe wa NHC uliofika Ofisini kwake kuhamasisha Halmashauri za Wilaya kusaidia vikundi vya vijana vilivyopewa msaada wa mashine za kufyatulia matofali na NHC.


Vyombo vya habari vimehusishwa katika uhakiki huu na hapa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Newala Bw. Marx Kamaoni akiongea na waandishi wa habari kuelezea mkakati wa Halmashauri yake kusaidia vijana.

Kikundi cha Vijana cha For Energy Group kilichopo Wilayani Masasi kilitembelewa na baada ya kuridhishwa  na utendaji wake NHC ilikiongezea mashine mbili zilizopokonywa vikundi vingine vilivyoshindwa kuzitumia Wilayani Newala na Masasi Vijijini. Hii ni nyumba iliyojengwa na kikundi hicho Wilayani Masasi.
Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya akivionya  vikundi vya vijana  vya Nayoden na Mangaka Wilayani Nanyumbu waliokula fedha ya mtaji waliopewa na NHC ambapo aliamuru kuchukuliwa kwa mashine zao na kuwapa muda wa kujiandaa. Aliwataka kuziomba mashine hizo kwa maandishi watakapokuwa tayari kuzitumia. Mashine hizo zilifungiwa Ofisi ya Kata ya Mangaka kwa muda wa miezi nane wakisubiri kupata fedha nyingine kutoka NHC.

Mashine iliyopokonywa vijana wazembe Wilayani Nanyumbu ikipandishwa katika gari baada ya vijana hao kuzembea kuitumia na kuifungia Ofisi kwa muda mrefu.
Uhakiki wa vikundi vya vijana vilivyopewa msaada wa mashine na NHC ili kujiajiri na kusaidia wananchi kupata matofali ya kujengea nyumba bora umeanza katika Mikoa mbalimbali ukianzia na Mkoa wa Lindi na Mtwara. Katika hali isiyotarajiwa Mkoa wa Mtwara ambao kwa muda mrefu umekuwa ukililia kuletewa maendeleo umeshindwa kutumia fursa ya msaada wa mashine kwa vijana waliyopewa na NHC hali iliyolifanya Shirika kutwaa baadhi ya mashine ili zipewe vikundi vingine vinavyofanya vizuri Fuatilia kupitia habari picha hizi ili ufahamu kilichojiri katika mikoa hiyo ya kusini mwa Tanzania. Leo uhakiki huo unaendelea Mkoani Ruvuma.

No comments: