Wednesday, June 24, 2015

KAMATI ZA MAAFA ZA TAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WAO WA MENEJIMENTI YA MAAFA

01
Mratibu Maafa, Idara ya uratibu maafa,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Benedict
Kisaka akitoa mafunzo ya menejimenti ya maafa wakati wa mafunzo kwa
waratibu maafa mkoani Kagera tarehe 24 Juni, 2015.
02
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Kagera, Fikira Kisimba (katikati)
akifuatilia mafunzo ya menejimenti ya maafa wakati wa mafunzo kwa
waratibu maafa mkoani Kagera tarehe 24 Juni, 2015, (mwenye miwani) ni
Mkurugenzi msaidizi (Mipango na Utafiti), Idara ya Uratibu maafa Ofisi
ya Waziri Mkuu, Naima Mrisho.
03
Mwakilishi wa  Mkuu wa Polisi wilaya ya Bukoba, Mkaguzi John Kayunga
akifafanua masuala ya menejimenti ya maafa katika Jeshi la Polisi
mkoani Kagera wakati wa  mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa waratibu
maafa mkoani Kagera.
04
Mratibu maafa wilayani Muleba Mkoani Kagera, Ruth Ishabakaki
akifafanua masuala ya menejimenti ya maafa wilayani Muleba wakati wa
mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa waratibu maafa mkoani Kagera
tarehe 24 Juni, 2015, mafunzo hayo yameratibiwa na Idara ya Uratibu
maafa Ofisi ya Waziri Mkuu.
05
Baadhi ya waratibu Maafa mkoani Kagera wakifuatilia mafunzo ya
menejimenti ya maafa kwa waratibu hao tarehe 24 Juni, 2015, mafunzo
hayo yameratibiwa na Idara ya Uratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu.
…………………………………….
Na. Mwandishi Maalum
Kamati za kuratibu maafa katika ngazi ya serikali za mitaa zimetakiwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ya menejimenti ya maafa ili kuweza kujenga jamii yenye uwezo wa kuzuia na kukabili maafa yanayotokea katika maeneo yao.
Akifungua mafunzo ya waratibu wa maafa mkoani Kagera, tarehe 24 Juni, 2015, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo, Fikira Kisimba alieleza kuwa nguvu ya uwezo wa jamii kuweza kukabili maafa itapatikana iwapo kamati za kuratibu maafa katika ngazi za serikali za mitaa zitawajibika wakati wote kwa kutokuwa zinasubiri uratibu wa maafa yanapotokea . 
“Tunazo kamati za maafa kuanzia ngazi za vijiji , vitongoji, kata , wilayani hadi mkoani lakini kamati hizi zinasikika sana wakati maafa yanapotokea hali ambayo si nzuri katika hatua za menejimenti ya maafa, kwani tunaposema menejimenti ya maafa tunazingatia, kuzuia, kukabili maafa na kurejesha hali ya awali baada ya maafa kutokea” alisema Kisimba.
Kisimba aliongeza kuwa mkoa wa Kagera umekuwa ukikumbwa na maafa ya upepo mkali ambapo alibainisha kuwa wilaya ya Muleba imewahi kupatwa na maafa hayo pamoja na maafa ya Kimbunga katika kisiwa cha Goziba lakini wilayani Misenyi magonjwa ya mlipuko yamekuwa yakijitokeza hivyo kamati husika zikiwajibika athari za maafa haya zinapunguzika.
Awali akiongea katika mafunzo hayo, Mkurugenzi msaidizi (Mipango na Utafiti), Idara ya Uratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Naima Mrisho alizitaka kamati za serikali za mitaa na vijiji mkoani humo kuhusisha maafa na mipango yao ya maendeleo, ili kuhakikisha jamii inakuwa na uwezo wa kupunguza athari za maafa hayo.
“Ili kamati za maafa ziweze kuwajibika ipasavyo hatunabudi Mipango ya maendeleo katika serikali za mitaa ihusishe maafa ili jamii iwe na uwezo wa kukabiliana na maafa wakati janga linapotokea na wakati wa kurejesha hali. Kamati za ” alisisitiza Mrisho.
Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Idara ya Uratibu Maafa itaendelea kutoa elimu na kushirikisha Wadau ili kuimarisha uwezo wa nchi katika kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana na athari za maafa yanapotokea.

No comments: