Thursday, June 18, 2015

Jaji Ramadhani achomoza urais





*Achukua fomu CCM na kusema; “Chema chajiuza

*Atamba ana uwezo wa kutosha kuiongoza nchi

*Ni nguli wa sheria,  mwanajeshi na kiongozi wa dini




JAJI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhani (70) ambaye kwa sasa ni Rais wa Mahakama ya Afrika, amepandisha joto la urais ndani ya CCM, baada ya jana kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Mara baada ya kuchukua fomu, Jaji Ramadhani ambaye pia ni mwanajeshi aliyestaafu akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali, kiongozi wa dini akiwa Mchungaji wa Kanisa Anglikana na mwanamichezo mahiri, alisema amejitokeza kwa kuwa ana uwezo wa kutosha katika kuongoza nchi.

Pia ameahidi kuyaangalia mapendekezo ya wananchi yaliyoachwa kwenye Katiba inayopendekezwa iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi kwani katiba ni ya wananchi.

"Sina makeke ndiyo maana nimeongozana na watu wachache kuja kuchukua fomu, siku zote chema chajiuza," alisema.

Alisema yeye ni mtu safi na hajawahi kutajwa mahali popote kuhusika na ufisadi kutokana na kuwa na mapenzi wa kuitumikia nchi yake na atahakikisha anashughulika na tatizo la rushwa na ufisadi katika nchi.

Akiwa ameongozana na mkewe, Saada Mbarouk Ramadhani ambaye ni mwanajeshi wa ngazi ya juu mwenye cheo cha Luteni Kanali, alisema ana uzoefu wa kutosha ndio maana anaomba dhamana ya chama na wananchi ili aweze kuwa kiongozi mkuu wa nchi.


"Nina vigezo vya kutosha na nia uwezo najiamini, nataka nipate nafasi ya kuteuliwa na chama na baadaye niwe kiongozi mkuu wa Nchi  ili kwa pamoja tuijenge nchi yetu," alisema

Jaji Mstaafu Ramadhani, tofauti na wagombea wengine zaidi ya 35 waliomtangulia kuchukua fomu CCM, hakujieleza, bali alitaka kuulizwa tu maswali na waandishi wa habari.

"Mimi sikuitisha kikao cha kutangaza nia ninataka waandishi waniulize maswali tu," alisema.

Alipoulizwa kama anaona kuna mgombea yeyote ambaye ni tishio kwake alisema, yeye ni Brigedia Jenerali hawezi kuogopa chochote.

Pia alipohojiwa akiwa rais atawezaje kuondoa tatizo la rushwa na ufisadi  na hata tatizo la mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, alisema matatizo hayo yote yatatafutiwa dawa mapema kwani hata alipokuwa Jaji Mkuu alizunguka mikoa 15 ambapo alikutana na wakuu wa mikoa na wilaya na walizungumzia suala hilo.

"Suala la rushwa na ufisadi ni mtoto pacha sheria zipo ni utekelezaji tu unaotakiwa," alisema.

Alisema tatizo la mauaji ya walemavu wa ngozi serikali inajitahidi na wale waliohusika wamefikishwa mahakamani wengine wamehukumiwa adhabu ya kifo na kinachosubiriwa ni utekelezaji wa adhabu hizo.

Alisema elimu zaidi inatakiwa kutolewa ili wananchi wafahamu viungo vya albino havileti utajiri.

Pia alipohojiwa kwamba, wakati akiwa kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba kuna mapendekezo ya wananchi yaliachwa, atafanyaje akipata nafasi ya kuongoza nchi?

Alijibu kwa kusema Katiba ni ya wananchi si ya kwake, na atasikiliza matakwa ya wananchi kama wakihitaji yarudishwe basi yatarudishwa.

Alipohojiwa amekuwa mwanachama wa CCM tangu lini alisema ameingia kwenye siasa mwaka 1969. Alisema alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa TANU tangu Agosti, mwaka 1969 wakati huo akiwa mwanafunzi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.






Akiwa chuoni wakati akikaribia kumaliza shahada yake akatuma maombi ya kujiunga na jeshi na na akaulizwa kama ni mwanachama wa TANU akasema ni mwanachama wa Vijana wa TANU akaambiwa lazima awe mwanachama wa Tanu ndipo ajiunge na Jeshi.

Alisema alikwenda kufuatilia kadi ya TANU na alifanikiwa kuipata na aliendelea kuwa na mwanachama wa CCM hadi mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipoanza na Katiba kukataza Majaji kuwa wanachama wa vyama vya siasa.

Jaji Mstaafu Ramadhani alisema alipostaafu Ujaji mwaka 2011 alirudi tena na kuwa mwanachama wa CCM. Pia  alipopata tu shahada ya chuo kikuu alijiunga na jeshi moja kwa moja na mwaka 1971 aliteuliwa kuwa Luteni Usu kwa alikaa makao makuu ya Jeshi na ilipoanzishwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora.

Alisema  Rais wa Zanzibar wakati huo, Mzee Aboud Jumbe alimuita arudi Zanzibar ili awe mwanasheria mkuu  lakini alitaka kujifunza kwanza kabla ya kushika nafasi hiyo.

Mwaka 1978 akawa Naibu Jaji Mkuu wa Zanzibar na wakati wa Vita baina ya Tanzania na Uganda alikwenda vitani na alirejea Zanzibar mwishoni mwa mwaka 1979 na ndipo akateuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Alipotoka Zanzibar aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Nchini kwa miaka 20, baadaye Jaji Mkuu miaka mitatu na nusu akastaafu na sasa ni Rais wa wa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika.
Historia yake
Jaji Augustino Ramadhani alizaliwa Desemba 28, 1945 mjini Unguja, Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya wanane waliozaliwa kwa wazazi wake. Baba yake ni Mathew Douglas Ramadhani, raia wa Zanzibar aliyefariki dunia mwaka 1962 na mama yake, Bridget Ramadhani alifariki dunia mapema mwaka huu.
Watu wengi hushangaa kuona au kusikia ana majina mawili ya dini tofauti. Augustino (jina la Kikristo) na Ramadhani (jina la Kiislamu). Lakini ukweli wa mambo ni kuwa yeye ni Mkristo wa dhehebu la Anglikana na ni mchungaji wa kanisa hilo.
Elimu ya msingi aliianzia wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma katika Shule ya Msingi Mpwapwa mwaka 1952 -1953 darasa la kwanza na la pili. Baadaye alihamia mkoani Tabora na kusoma darasa la tatu na la nne katika Shule ya Mingi “Town School” mwaka 1954 – 1956. Mwaka 1957 – 1958 alisoma darasa la la sita na la saba katika Shule ya Msingi Kazel Hill (sasa inaitwa Shule ya Msingi Itetemia), kabla ya kurudi Mpwapwa ambako alikamilisha darasa la nane mwaka 1959.
Aijiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora mwaka 1960-1965 kwa ajili ya elimu ya kidato cha kwanza na nne pamoja na elimu ya kidato cha tano na sita. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alipata fursa ya kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akianza kusomea Sheria. Shahada hii nyeti aliisoma kuanzia mwaka 1966 hadi alipohitimu Machi 1970 na baada ya kuhitimu alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria na aliajiriwa katika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kufanya kazi za uanasheria.
Kwa mtu mwenye shahada ya chuo kikuu enzi za miaka ya 1970, kupanda vyeo kilikuwa kitu cha lazima. Jeshi halikuwa na wasomi wengi kama ilivyokuwa katika sekta nyingine na kila aliyekuwa na elimu kubwa alikuwa mtu muhimu.
Ndiyo maana haikushangaza kwamba mwaka 1971 tayari alikuwa Luteni (nyota mbili) akiwa kambi ya Mgulani na miaka sita baadaye akahamishiwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora wakati huo akiwa tayari ni Meja.
Kutoka hapo, alifanya kazi jeshi na uraiani kwa vipindi tofauti hadi alipostaafu na sasa kujiona ameshakomaa katika nyanja nyingi, hivyo yuko tayari kuvaa viatu vya Rais wa Awamu ya Nne anayemaliza muda wake, Rais Jakaya Kikwete.
Anakuwa Mzanzibari wa tatu kujitosa Urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania mwaka huu, wengine wakiwa Mtoto wa Mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Ali Karume na mwanadiplomasia aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Amina Salum Ali ambaye kwa sasa ni Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) huko Marekani.
SOURCE: Sifa Lubasi, HabariLEO Dodoma

No comments: