TOVUTI KUU YA SERIKALI YAZINDULIWA RASMI, TAARIFA NA HUDUMA MBALIMBALI SASA KUPATIKANA KWA NJIA YA MTANDAO



Waziri Mkuu Mizengo Pinda (katikati) akiwa ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Celina Kombani wakiwasili katika Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao kupata maelezo ya Tovuti Kuu ya Serikali kabla ya kuizindua tovuti hiyo  jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tovuti Kuu ya Serikali www.tanzania.go.tz itakayowawezesha wananchi kupata taarifa na huduma mbalimbali za serikali kwa urahisi, haraka na kwa wakati. Wanaoshuhudia kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Celina Kombani na Dkt. Jabiri Bakari ,Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao ambao ni wasimamizi wa Tovuti hiyo.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akifurahia jambo mara baada ya kuzindua Tovuti Kuu ya Serikali na kuwataka wananchi kuitumia katika kupata taarifa mbalimbali za serikali.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akipata maelezo kuhusu uundwaji wa Tovuti Kuu ya Serikali na namna inavyoendeshwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Msaidizi wa Mifumo Shirikishi ya Umma Bw. Fratern Hassani (kulia) katika Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao wasimamizi wa Tovuti Kuu ya Serikali. Wengine wanaosikiliza kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Jabiri Bakari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Celina Kombani,Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa, Makatibu wakuu na watendaji wengine wa serikali.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akizungumza jambo mara baada ya kupata maelezo kuhusu mifumo ya uendeshaji wa Tovuti Kuu ya Serikali alipokutana na wataalam wanaosimamia Tovuti hiyo katika Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao jijini Dar es saalam. Picha na 6. Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakitekeleza makumu yao wakati wa uzinduzi wa Tovuti Kuu ya serikali katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Bakari akitoa ufafanuzi kwa wadau mbalimbali juu ya wa namna Tovuti Kuu ya Serikali inavyofanya kazi na namna ya kupata taarifa za serikali wakati wa uzinduzi wa Tovuti hiyo jijini Dar es salaam.
Wafanyakazi wa Wakala ya Serikali Mtandao waliofanikisha uzinduzi wa Tovuti Kuu ya serikali.
Baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambayo ndiyo msimamizi wa maudhui ya Tovuti Kuu ya Serikali kupitia Idara ya Habari –MAELEZO waliohudhuria Uzinduzi wa Tovuti Kuu hiyo.Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Bw. Raphael Hokororo akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene.
Waandishi wa habari wakiwajibika. Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.

Na. Aron Msigwa – MAELEZO,Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda amesema kuwa kuanzia sasa wananchi wanaweza kupata taarifa na huduma mbalimbali za serikali kwa urahisi zaidi  kwa njia ya mtandao katika maeneo wanayoishi bila hata kulazimika kufika kwenye ofisi husika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tovuti Kuu ya Serikali jana jioni jijini Dar es salaam, Mh Pinda amesema kuwa tovuti kuu ya serikali sasa itawawezesha wananchi kupata taarifa ya huduma mbalimbali za serikali na namna ya kupata huduma hizo kwa njia ya mtandao na kupunguza usumbufu wa kulazimika kusafiri eneo moja hadi jingine kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali.

 Alisema tovuti hiyo inayopatikana sasa kwa anuani ya www.tanzania.go.tz ni mojawapo  ya juhudi za Serikali  katika kuhakikisha kuwa taarifa na huduma zinazotolewa na Serikali zinapatikana na kuwafikia wananchi kwa urahisi,  wakati wowote na mahali popote ndani na nje ya nchi.

Alieleza kuwa tovuti  hiyo  ni moja ya mafanikio makubwa katika kutimiza dira ya muda mrefu ya kuwa na dirisha moja linalotoa taarifa na huduma zinazotolewa na Taasisi  za Serikali kwa urahisi na kuongeza kuwa licha ya kurahisisha upatikanaji wa taarifa itawapunguzia Wananchi usumbufu kwa kuokoa muda wa kufuatilia taarifa hizo kutoka eneo moja hadi jingine.

Alisema kuwa taarifa za masuala mbalimbali kuhusu Kilimo, Biashara, Viwanda, Ufugaji, Masoko, Elimu na nyingi zinazohusu taifa la Tanzania sasa zinapatikana kupitia Tovuti Kuu ya Serikali na kutoa wito kwa wananchi kuitumia tovuti hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Celina Kombani akizungumza wakati wa uzinduzi huo alisema kuwa uzinduzi huo umekuja kwa wakati muafaka kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya taarifa mbalimbali za serikali zinazowahusu wananchi katika masuala ya biashara, uwekezaji, kilimo, ufugaji, uhamiaji, nishati na madini na masuala mengine yanayohusu maisha ya kila siku.

Alisema kuwa Menejimenti ya Utumishi wa Umma itaendelea kufanya kazi bega kwa beg na Wakala ya serikali Mtandao kuhakikisha inaijengea uwezo ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo ya kuwahudumia wananchi.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao ambao ndio wasimamizi wa tovuti hiyo Dkt. Jabiri Bakari akizungumza wakati wa uzinduzi huo alisema kuwa Wakala ya serikali anayoisimamia itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali  katika kutoa huduma zake kwa wananchi.

Alisema wakala kwa kushirikiana na Wizara, taasisi, mikoa na Halmashauri za wilaya itaweza kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha kuwa taarifa za serikali zinapatikana kwa urahisi na kwa kuzingatia muda na kuongeza kuwa italitekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Idara ya Habari –MAELEZO ambao ndio wasimamizi wa maudhui wa tovuti hiyo.

 Kuhusu taarifa na huduma zilizomo katika Tovuti Kuu ya serikali Dkt. Jabiri alisema zimegawanywa katika maeneo makuu sita ambayo ni Serikali, Wananchi, Taifa letu, biashara, Sekta na Mambo ya Nje.

Alisema maeneo yote yanalenga kurahisha utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za upatikanaji wa nyaraka zote za Serikali, huduma zinazotolewa na Serikali kwa njia ya simu na mtandao, Viwango vya fedha, Hali ya Hewa, na Soko la Hisa.

Alisema huduma nyingine katika Tovuti Kuu hiyo imetengwa katika ukarasa wa Nifanyeje unaopatikana ndani ya tovuti hiyo ambao  unamjengea uwezo mwananchi kufahamu taratibu za upatikanaji wa huduma zinazotolewa na taasisi mbali mbali za Serikali kama upataji wa hati ya kusafiria, kibali kazi, TIN, cheti cha kuzaliwa na mikopo ya vyuo.

Aliongeza kuwa tovuti hiyo pia inalenga kuziunganisha Tovuti na mifumo ya Taasisi mbali mbali inayotoa taarifa na huduma kwa wananchi na wafanyabiashara katika dirisha moja.

Tovuti Kuu hiyo ilianza kutengenezwa mwaka 2009 na kupatikana kwa anuani ya www.egov.go.tz chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Tovuti hiyo iliboreshwa na kuunganishwa na iliyokuwa Tovuti ya Taifa kwa anuani ya www.tanzania.go.tz  mwaka 2012 chini ya Wakala ya Serikali Mtandao.

Comments