WANARIADHA kutoka nchi 21 wanatarajiwa kushiriki mbio ndefu za Uhuru, Uhuru Marathon, zinazotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Desemba 8, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, kujitokeza kwa wanariadha kutoka mataifa mbalimbali kumeongeza hamasa kubwa ya mbio hizo.
Melleck alisema, wanariadha kutoka mataifa hayo ndio ambao wamejiandikisha mpaka sasa na wanaamini wengi wataendelea kujitokeza ili kufanikisha lengo lake.
Alitaja nchi wanazotoka wanariadha waliojiandikisha mpaka sasa ni Tanzania, Uganda, Kenya, Afrika Kusini, Ethiopia, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi na Marekani.
Wanariadha wengine wanatoka Ujerumani, Jamaica, Urusi, China, Japan, Venezuela, Comoro, Nigeria, Italia, Canada, Madagascar na Uturuki.
“Hii ni faraja kubwa kwetu, kwani inaonyesha kwa kiwango kikubwa lengo letu la kupigania amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu linakubalika na watu wengi duniani,” alisema.
Aidha Melleck alise,a usajili bado unaendelea kwa wale wanaotaka kushiriki ambapo fomu zitakazotolewa kwa mshiriki wa kilomita 3 atalipa Sh 100,000 yule wa kilomita 5 Sh 2,000 na washiriki wa kilomita 21 na 42 watalipia Sh 6,000.
“Tunachukua nafasi hii pia kuziomba kampuni au taasisi mbalimbali zinazotaka kudhamini mbio hizo zijitokeze na kufanya hivyo, kwani nafasi bado ipo na tukumbuke bila amani hakuna chochote kinachoweza kufanyika,” alisema.
Comments