Tuesday, March 03, 2015

HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2015, YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ILIYOTOLEWA TAREHE 1 MACHI, 2015

17
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuzungumza kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa hotuba za kila mwisho wa mwezi. Kwa mwisho wa mwezi wa Februari nina mambo matano ninayopenda kuyazungumzia. 
Zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura
Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni uandikishaji wa Wapiga Kura. Tarehe 24 Februari, 2015 Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda alizindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura ikiwa ni sehemu ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini. Zoezi hili lilizinduliwa Makambako, Mkoani Njombe na litaendelea nchini kote mpaka litakapokamilika kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa na Tume ya Uchaguzi. Uandikishaji unatumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa alama za vidole (BVR) na macho ya mtu anayeandikishwa. Teknolojia hii itatusaidia kuondoa kutoaminiana, manung’uniko na madai kuhusu udanganyifu katika chaguzi zetu kwamba wamepiga kura wasiostahili. Kuanza kutumika kwa teknolojia hii ni kielelezo cha utashi wa Serikali kuwa nchi yetu iwe na chaguzi zilizo huru, wazi na haki.
Ndugu Wananchi;
Mtakumbuka kuwa, kabla ya uzinduzi wa zoezi hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya zoezi la majaribio ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mashine za teknolojia hii mpya katika kata 10 katika Halmashauri za Kinondoni, Kilombero na Mlele kati ya tarehe 15 hadi 23 Desemba, 2014. 
Habari njema ni kuwa, kwa kutumia mashine za BVR, idadi ya waliojiandikisha ilivuka lengo la uandikishaji kwa kipindi kilichopangwa katika Kata hizo. Katika Halmashauri ya Kilombero walioandikishwa walifikia asilimia 110.9 ya lengo, katika Halmashauri ya Mlele uandikishaji ulifikia asilimia 101 ya lengo na katika Jimbo la Kawe, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni walioandikishwa walikuwa asilimia 105.67 ya lengo. Mafanikio haya ni ya kutia moyo pamoja na changamoto za kiufundi zilizojitokeza na zile zinazotokana na upya wa mfumo wenyewe kwa watumiaji. Changamoto hizo zimefanyiwa kazi na watengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji wa wapiga kura nchi nzima. 
Ndugu Wananchi; 
Nimefarijika na taarifa kuwa zoezi la uboreshaji wa Daftari na uandikishaji wa wapiga kura limeanza vizuri Makambako. Wananchi wamejitokeza kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa. Kati ya tarehe 23 hadi 25 Februari, 2015 kwa mfano, Tume ilitegemea kuandikisha wapiga kura 9,541 lakini kutokana na mwamko wa wananchi kuwa mkubwa wameweza kuandikisha wapiga kura 13,042. Kila kituo kilikuwa kinaandikisha kati ya wapiga kura 80 na 150 kwa siku. Lengo la Tume ni kuandikisha wapiga kura 32,000 katika Halmashauri ya Makambako ambako kwa siku wanatarajia kuandikisha watu 4,320. Naambiwa kuwa hesabu za juzi na jana wameandikisha hadi wapiga kura 6,000 kwa siku. Kwa kasi hii na kama mambo yatakwenda kama inavyotarajiwa, lengo hilo litafikiwa na hata kuvukwa.
Ndugu Wananchi;
Hatuna budi kutoa pongeza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa hatua hii ya kutia moyo tuliyofikia katika mchakato huu. Inaondoa hofu iliyoanza kuingia miongoni mwa baadhi ya watu kuwa huenda zoezi hili lisingefanikiwa. Tunachokitaka kwa Tume ni kuona zoezi hili linaendelea na kukamilika kama ilivyopangwa. Napenda kurudia ahadi niliyokwishaitoa kwa Tume kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana kuiwezesha kirasilimali ili iweze kutimiza jukumu lake hilo. Nimekwishawakumbusha Hazina kuhusu umuhimu wa zoezi hili kufanikiwa kama ilivyopangwa. Hivyo basi, nimewataka wahakikishe kutoa kipaumbele cha kwanza katika mgao wa fedha. Kama haifanyiki nawaomba Tume waniambie mimi mwenyewe.
Wito wangu kwenu, wananchi wenzangu, ni kujitokeza bila ya kukosa kwenda kujiandikisha kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji katika maeneo yenu kama itakavyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Msifanye ajizi maana hakutakuwepo na fursa nyingine ya kujiandikisha kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu baada ya fursa hii kupita. 
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyoelezwa na Tume na mimi kusisitiza mara kadhaa kuwa watakaojiandikisha wakati huu ndio watakaopiga kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na ndio watakaopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Vitambulisho vya zamani vya mpiga kura havitatumika, hivyo watu wote ambao ni Watanzania na wana umri wa miaka 18 au zaidi lazima wajitokeze kuandikishwa upya. Watu pekee ambao hawatapaswa kujiandikisha tena ni wale tu walioandikishwa katika zoezi la majaribio lililofanyika katika zile kata 10 za Halmashauri za Kinondoni, Ifakara na Mlele mwezi Desemba, 2014. Vitambulisho walivyopata ndivyo vyenyewe.

No comments: