Saturday, May 07, 2016

SERIKALI YABAINI TANI 4,579.2 ZILIZOKUWA ZIMEFICHWA KWENYE MAGHALA

indexFrank mvungi-Maelezo
Taasisi ya kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) yabaini kuwepo kwa sukari iliyofichwa  tani 4,579.2 iliyonunuliwa toka Kiwanda cha Sukari Kilombero.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Valentine Mlolowa Taasisi  hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya swala hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa mnamo tarehe 05 Mei, 2016 timu ya uchunguzi ilitembelea maghala yaliyopo Tabata Jijini Dar es salaam na kubaini uwepo wa sukari hiyo.
 TAKUKURU tayari imetembelea  Maghala ya mfanyabiasha Haruni Daudi Zacharia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Al-Naeem yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa sukari hapa nchini na anayetuhumiwa kuficha bidhaa hiyo. Ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha uchunguzi  uliofanywa na Taasisi hiyo ulibaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza  sukari iliyokutwa katika maghala hayo kulikofanywa na mfanyabiashara huyo kwani hata sehemu ya Maghala ilipo sukari hiyo hapakuwa na dalili za upakiaji wa sukari  hiyo ili iweze kusambazwa.
Taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa katika eneo la Kitumbini  kumekuwa na wananchi wengi wanaohitaji  bidhaa hiyo na wachache sana waliweza kuuziwa  licha ya ukweli kwamba sukari ilikuwepo.
Katika uchunguzi wake TAKUKURU pia  imebaini kuwepo kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na mfanyabiasha huyo kwa kununua sukari yote toka viwanda vya ndani na kisha kuihifadhi na kuuza bidhaa hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku wakati alikuwa na uwezo wa kuuza zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari katika soko.
Kuficha bidhaa ni kosa la uhujumu uchumi na ni  kinyume na Aya ya 3 Jedwali la kwanza Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 [Chapisho la Mwaka 2002]. Serikali haitavumilia hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote ataekwenda kinyume na sheria hii.
TAKUKURU  imetoa wito kwa wafanyabiashara wote wa sukari kuacha vitendo vya kuficha sukari na vyombo vya uchunguzi vinafuatilia kote nchini na yeyote atakayebainika kufanya hujuma hizo atakabiliwa na mkondo wa Sheria.

No comments: