Thursday, May 05, 2016

NHIF YAZINDUA HUDUMA TOTO AFYA KADI

 Meneja Huduma za Dawa Michael Kishiwa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ( NHIF)  akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu huduma mpya ya mfuko huo iitwayo “Toto Afya Kadi” inayohusisha watoto wenye umri chini ya miaka kumi na nane ambao sio wanachama wa kundi la mwajiriwa, Kushoto ni Afisa Masoko wa Mfuko huo Bi. Sabina Komba.
Baadhi ya waandishiwa Habari wakifuatilia mkutano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)  umepanua huduma za mfuko wake kwa kuanzisha huduma mpya iitwayo “Toto Afya Kadi”.Hayo yameelezwa na Meneja Huduma za Dawa NHIF Michael Kishiwa leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.

“Huduma ya Toto Afya Kadi ni huduma ambayo inahusisha watoto chini wenye umri chini ya miaka kumi na nane ambao sio wanachama wa kundi la mwajiriwa kwa mwajiri hasa wale ambao wanalelewa katika vituo vya watoto yatima au wanaolelewa na ndugu waliokosa fursa ya kujiunga na huduma ya Bima ya Afya,” alisema Kishiwa.

Kishiwa alisema kuwa, mwanachama ambaye ni mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 atatakiwa kujaza fomu zinazopatikana nchi nzima chini ya uangalizi wa mdhamini ambaye ni mlezi wake aidha kwenye kituo anacholelewa au mahali anapoishi.

Aidha, Kawishe alisema kuwa mwanachama wa Toto Afya Kadi atapata huduma zote ambazo mwanachama wa huduma ya Bima ya Afya ya NHIF anapata na ambazo zimeorodheshwa katika huduma ambazo zinatolewa na Bima hiyo kwa gharama ya shilingi 50,400 kwa mwaka.

Pia alisema kwa kijana ambaye amepita miaka 18 ili kuweza kuendelea kuwa mwanachama wa Bima ya Afya na hajaajiriwa atatakiwa kujiunga katika vikundi vilivyosajiliwa ili aweze kusajiliwa katika mfumo wa kikoi kwa kuchangia kiasi cha shilingi 76,800 kwa mwaka.

NHIF ina wanachama asilimia 12 ya watanzania huku ikiwa na jumla ya vituo 6700 nchi nzima, na mpaka sasa jumla ya wanachama 2,000 wa Toto Afya kadi wamesajiliwa nchi nzima tangu ianze Machi, 2016.
Post a Comment