Tuesday, May 24, 2016

CBE YATOA UFAFANUZI TUHUMA ZA UPOSTOSHAJI.

 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emmanuel Mjema akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) ripoti ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) inayoonesha kuwa chuo hicho kimepata ziada ya bilioni 1.2 kati ya mwaka huu na kufanya chuo kujiendesha kwa faida tofauti na baadhi taarifa za upotoshaji zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari.
 Mkuu wa Chuo cha Elimu Biashara (CBE) Prof. Emmanuel Mjema akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ya Mwaka huu inayoonesha chuo hicho ni moja kati ya Taasisi 14 zilizofanya vizuri kwa kushika nafasi ya kwanza kwa kupata alama 95.8 katika kufuatilia sheria ya manunuzi ya umma na kuutaka umma kupuuza taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa wanakiuka sheria hizo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo.PICHA NA HASSAN SILAYO-MAELEZO

Frank Mvungi-Maelezo

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimewataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji zilizoripotiwa na Baadhi ya vyombo vya Habari Hapa nchini kuhusu chuo hicho.

Akizungumza na vyombo vya Habari leo jijini Dar es salaam Mkuu wa chuo hicho Prof. Emmanuel Mjema amesema tuhuma za kuwa chuo hicho kina ubadhirifu wa kutisha si za kweli na zinalenga kuchafua taswira ya chuo hicho.

“Chuo kinafanyiwa ukaguzi wa Hesabu zake na Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali na kwa kipindi cha miaka minne tumepata hati safi (clean audit report) kuanzia mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015 .” alisisitiza Prof. Mjema.

Katika ukaguzi huo ripoti hiyo ilionyesha kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikizingatia sheria na kanuni za matumizi ya fedha za umma hali iliyopelekea kupata hati safi kwa kipindi chote.

Pia Chuo hicho kilifanyiwa ukaguzi na Mamlaka ya Udhibiti wa manunuzi Serikalini (PPRA) kwa mwaka unaoishia 2014/2015 na Chuo hicho kupata alama 95.8 hivyo kuwa moja ya Taasisi za Umma zinazofanya vizuri katika kuzingatia sheria na kanuni za manunuzi ya umma.

Prof. Mjema amesema kuwa chuo hicho kimekuwa kikijiendesha bila kupata ruzuku toka Serikalini na pia kuzalisha mapato ya ziada zaidi ya bilioni moja kwa kwa kila mwaka wa fedha kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.

Kutokana na Mafanikio hayo chuo hicho kimeweza kuanzisha Kampasi ya Mbeya ambapo chuo hicho kimenunua eneo lenye ukubwa wa ekari 54.9 na pia maboresho katika maktaba ya chuo yamefanyika.

Mafanikio mengine ni kujenga hema kubwa lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 740 na kuboresha karakana ya vipimo na mizani chuoni hapo.

No comments: