Tuesday, May 31, 2016

BALOZI HERBERT MRANGO AKAGUA UKARABATI MV MAGOGONI

 Mkurugenzi wa Uzalishaji na Matengenezo TEMESA Mhandisi Silvester Simfukwe (katikati walio chuchumaa) akiwaonesha Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) sehemu ya kivuko cha Magogoni inayoendelea kufanyiwa ukarabati.
Kivuko cha Magogoni kikiwa katika ukarabati katika Bandari ya Dar es Salaam.Picha na Theresia Mwami-TEMESA.
 Kaimu Mtendaji wa TEMESA Mhandisi Manase Ole kujan (Kushoto) akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme(TEMESA) Balozi Herbert Mrango (katikati) wakati Bodi hiyo ilipotembele ukarabati wa kivuko cha magogoni.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme(TEMESA) Balozi Herbert Mrango( wa tatu kulia) akiongoza na wajumbe wa bodi hiyo wakati Bodi hiyo ilipotembele ukarabati wa kivuko cha magogoni.
Na Theresia Mwami- TEMESA

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imetembelea na kujionea maendeleo ya ukarabati wa kivuko cha Mv Magogoni chini ya kampuni ya Songoro Marine katika Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi Herbert Mrango ameeleza kuridhishwa na kasi ya ukarabati wa kivuko hicho na kuushauri uongozi wa TEMESA kuharakisha malipo yanafanyika kwa wakati ili kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa.

“Nakuagiza Kaimu Mtendaji uhakikishe malipo kwa kampuni hii yanafanywa kwa wakati na ukarabati huu kukamilika mapema ili kuwapa fursa wananchi kutumia kivuko hiki”alisema Balozi Mrango.

Aliongeza kuwa ni muhimu wananchi kurejeshewa huduma ya kivuko hicho ili kuondoa kero inayowakabili kwa sasa kwa kuwa na kivuko kimoja chenye uwezo wa kubeba magari ambapo kukamilika kwa ukarabati wa huu utakuwa umerahisiha shughuli ya usafirishaji.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji wa TEMESA Mhandisi Manase Ole kujan amesema atahakikisha malipo yanafanyika kwa wakati ili kuwezesha mkandarasi huyo kumaliza kazi hiyo kwa muda uliopangwa na kurejesha huduma ya kivuko hicho kwa wananchi.

Aidha aliongeza kuwa kazi ya ukarabati wa kivuko hicho imegawanywa katika sehemu mbili ambazo ni, ukarabati wa “Body” pamoja na mifumo ya umeme unaofanywa na Mkandarasi kutoka kampuni ya Songoro Marine huku TEMESA ikihusika na ukarabati wa mitambo ya kuongozea kivuko.

Kivuko cha Mv Magogoni kinachotoa huduma katika maeneo ya kigamboni na Magogoni Jijini Dar es Salaam kilisimamisha rasmi kutoa huduma hiyo mapema Mei mwaka huu kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa chini ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na kampuni ya Songoro Marine kukiongezea ufanisi katika kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi.

No comments: