Monday, March 02, 2026

TANZANIA NA GHANA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA AJIRA KWA VIJANA

Arusha, 02 Machi 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mazungumzo ya pande mbili na Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mheshimiwa John Dramani Mahama, Ikulu ya Arusha, yakilenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika sekta za uchumi, ajira kwa vijana na maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu mazungumzo hayo yamejikita katika kuongeza thamani ya rasilimali za ndani badala ya kuendelea kuuza malighafi, sambamba na kukuza mageuzi ya viwanda na biashara kati ya nchi hizo mbili. 

Viongozi hao wameonesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha usimamizi wa sekta za madini na mazao ya kimkakati kama kakao na pamba, kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani na kuchochea uchakataji wa ndani.

Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuharakisha mkakati wa uchumi wa viwanda, ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya kimkakati na kuimarisha uchakataji wa madini. 

Ameeleza kuwa uzoefu wa Ghana katika usimamizi wa rasilimali na sera za uchumi wa ndani ni fursa muhimu ya kujifunza na kushirikiana kwa maslahi mapana ya mataifa hayo mawili.

Kuhusu ajira kwa vijana, Marais hao wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika nyanja za ujuzi, ubunifu na ujasiriamali, pamoja na kuweka mazingira bora ya uwekezaji yatakayochochea ajira endelevu. Msisitizo umewekwa katika kukuza sekta za teknolojia, ubunifu wa kidijitali na huduma za kifedha ili kuongeza ushindani wa kiuchumi.

Katika eneo la TEHAMA, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali na kuimarisha usalama wa mitandao. Amebainisha kuwa uzoefu wa Ghana katika teknolojia ya fedha na ulinzi wa miundombinu ya kimtandao ni eneo la kimkakati la ushirikiano, likiwa na lengo la kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na ufanisi wa huduma za kifedha.

Viongozi hao pia wamepongeza hatua ya kuimarisha usafiri wa anga kati ya nchi hizo mbili kupitia Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), wakieleza kuwa safari za moja kwa moja zitarahisisha biashara, utalii na mwingiliano wa wananchi, si tu kati ya Tanzania na Ghana bali pia katika ukanda wa Bara la Afrika.

Rais wa Ghana yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Leo, tarehe 02 Machi 2026, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama, pamoja na Maadhimisho ya Miaka 20 ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, yenye makao makuu jijini Arusha.







No comments:

TANZANIA NA GHANA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA AJIRA KWA VIJANA

Arusha, 02 Machi 2026 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mazungumzo ya pande mbili na Ra...