Wednesday, June 08, 2016

SERIKALI YATENGA BILIONI 11,820 KWA MIRADI YA MAENDELEO 2016/17

 Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akimpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Phillip Mpango mara baada ya kuwasilisha hotuba ya taaarifa ya hali ya uchumi 2015 na mpango wa maendeleo wa taifa 2016/17 mjini Dodoma .

Serikali imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 11,820.503 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2016/17.Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Philip Mpango wakati akitoa hotuba kuhusu taarifa ya hali ya uchumi nchini na mpango wa maendeleo wa taifa 2016/17.

Waziri Mpango amesema kuwa kiwango hicho ni sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ya serikali na kuongeza kuwa fedha za ndani ni shilingi bilioni 8,702.697 ambazo ni sawa na asiliia 74 ya bajeti ya maendeleo na fedha za nje ni shilingi bilioni 3,117.805 sawa na aslimia 26 ya maendeleo.Aidha, Mpango amesema kuwa sekta binafsi inatarajiwa kuwekeza kiwango kikubwa cha fedha ili kuanzisha na kuendeleza viwanda ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango huo.

“ Kwa ujumla fedha za maendeleo zimeelekezwa zaidi katika miradi inayolenga kuendeleza viwanda kama vile uchukuzi,ujenzi, nishati, kilimo, maji, elimu na afya,”amesema Waziri Mpango.

Ameongeza kuwa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 umeainisha miradi mikubwa ya kielelezo ambayo itapewa msisitizo katika utekelezaji wake.

Waziri Mpango ameitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma, mradi wa chuma Liganga, ujenzi wa reli mpya kati ya Dar – Kigoma na Tabora- Mwanza na matawi yake Isaka- Kigali/Keza- Msongati na Kaliua- Mpanda kwa kiwango cha standard gauge.

Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 utategemea zaidi ushiriki wa sekta binafsi.

No comments: