Wednesday, June 22, 2016

MAGARI YANAYOINGIZWA KWA MSAMAHA WA KODI KUWA NA NAMBA NA RANGI MAALUM

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma 

Katika kuthibiti matumizi ya magari yanayoingia Nchini kwa msamaha wa kodi Serikali imesema kuanzia Julai Mosi magari hayo sasa yatakuwa na namba na rangi maalum.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu tamko la kuondoa misamaha ya kodi kwenye taasisi za dini kwa kuwa zinatoa huduma za kijamii kama shule na hospitali.

“Kwa kutambuua mchango mkubwa wa Taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za elimu na afya, napendekeza kufuta utaratibu niliotangaza katika hotuba ya bajeti na badala yake Serikali itaimarisha zaidi hatua mbalimbali za uthibiti misamaha ya kodi ikiwemo magari yaliyoingia kwa msamaha wa kodi kuwa na namba na rangi maalum,” alifafanua Mhe.Dkt. Mpango.

Aliendelea kutaja hatua nyingine kuwa ni taasisi za kidini kuwasilisha vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa kutoka nje ya nchi kila mwazo mwa mwaka wa kalenda na kuthibitisha kama vifaa vilivyopewa msamaha mwaka uliopita vilitumika kama sheria inavyotaka.

Pia, kuwasilisha majina ya watu walioidhinishwa na Shirika au Taasisi kuandika barua ya kuomba msamaha wa kodi, wakiainisha cheo, saini, picha, anwani na namba zao za simu ili kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kufuatilia bidhaa zilizoombewa na kupewa msamaha kama zimepata kibali cha taasisi hizo.

Vile vile taasisi hizo zinatakiwa kupata barua kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa na Mkuu wa Wilaya mahali Taasisi au Mradi unaotekelezwa ulipo. Mhe. Mpango amesema kuwa hatua hizo zimekuja kutokana na bidhaa zinazoombewa msamaha wa kodi kutumika tofauti na kusudi la msamaha huo.

Aidha ametoa tahadhari kwa mashirika ya kidini kuanzia sasa, kuhakikisha kuwa yanafuata taratibu zote na Kuzingatia masharti ya msamaha unaotolewa ili kuepuka kufutiwa leseni zao pale zitakapokwenda kinyume na sheria na kanuni zilizowekwa.

No comments: