Tuesday, June 21, 2016

HUDUMA YA CHAKULA HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI YABORESHWA.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa MNH, Aligaesha akifafanua jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari LEO jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha akizungumza na waandishi wa habari LEO kuhusu hospitali hiyo kuanza kuboresha huduma ya chakula kwa wagonjwa (special diet) wanaolazwa MNH kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
 Mkurugenzi wa Uuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Agness Mtawa akifafanua jambo LEO katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu hospitali hiyo kuanza kuboresha huduma ya chakula kwa wagonjwa. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Aminiel Aligaesha akiwa kwenye mkutano huo. 

·         Yawaondolea usumbufu ndugu wa wagonjwa kupeleka  chakula mara tatu kwa siku.
·         Ndugu watapata muda wa kuendelea na shughuli za uzalishaji
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeboresha huduma za chakula kwa wagonjwa wote watakaolazwa kuanzia Julai Mosi, mwaka huu ili kuwaondolea ndugu wa wagonjwa usumbufu na gharama za usafiri wakati wa wanapokwenda kuwaona ndugu zao waliolazwa mara tatu kwa siku katika hospitali hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar Es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha amesema hospitali imeingia ubia na mzabuni ili kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa wote wanaolazwa.

Kwanini Hospitali imechukua hatua hii
Bw. Aligaesha amesema Hospitali inataka kujikita katika majukumu yake ya msingi ambayo ni kushauri, kuchunguza na kutibu.

“Aidha Hospitali inataka kuwaondelea adha ndugu wa wagonjwa ambao wamekuwa wakiingia gharama kubwa hususani usafiri wa kuja Hospitalini mara tatu kwa siku, ambapo kwa kukadiria gharama ya usafiri wa ndugu mmoja wa mgonjwa ni kati ya shilingi 6,000/= na 10,000/= kwa siku, kulingana na mahali anapotokea bila kujumuisha gharama za kuandaa chakula cha mgonjwa ambacho mara nyingi ni chakula maalumu. Na kama mgonjwa akilazwa zaidi ya siku tano hadi 10 ndugu mmoja wa mgonjwa gharama atalipia fedha nyingi kwenye usafiri” amesema Bw. Aligaesha



Ameongeza kuwa adha ya pili wanayopata ndugu ni usumbufu ambapo inabidi kuacha shughuli nyingine za uzalishaji ili kuja kuleta chakula mara tatu kwa siku, hivyo kuingiliana na shughuli zao za kiuchumi na kimandeleo na kushindwa kuzalisha. Hivyo jukumu hili linachukuliwa na Hospitali kuwaondolea adha hii.
“Pia kuna baadhi ya ndugu wamekuwa wakishindwa kuwaletea chakula wagonjwa wao hivyo hospitali ililazimika kuwapatia chakula ambacho kilikuwa kwa ajili ya wagonjwa wanaotoka mikoani wasio na ndugu hapa Dar Es Salaam” amesisitiza Bw. Aligaesha. 

Amesema kumekuwepo na ongezeko la msongamano wa watu ndani ya Hospitali toka asubuhi saa 12 mpaka saa 12 jioni, suala linaloingiliana na utoaji huduma hasa saa za mchana kwani muda wa saa 6.00 hadi saa 8.00 mchana ulikuwa unaingiliana na majukumu ya kiutendaji ambapo majopo mbalimbali ya watalaamu yamekuwa yakiendelea na raundi za wagonjwa waliolazwa. Hii wakati mwingine imesababisha mgonjwa kutokupata huduma stahiki kutokana na muingiliano huu.
·                      
“Vile vile msongamano huu ni changamoto kwa ajili ya masuala ya kiusalama ambapo kati ya watu wanaoingia Hospitali kwa kigezo cha kuja kuona wagonjwa kuna wanaoingia kwa lengo la kufanya uhalifu ikiwemo wizi wa mali za Hospitali, magari  pamoja na vifaa vya magari” alisisitiza.
               
 Amesema kwa kufanya hivyo, Hospitali itapunguza baadhi ya gharama za uagizaji wa vyakula kwa wazabuni, kulinda upotevu na baadhi ya vyakula kuharibika wakati mwingine kwani utunzaji wa vyakula una mahitaji makubwa.

  Bw. Aligaesha amesema Hospitali inakusudia kutoa chakula chenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa wagonjwa ikiwemo kutoa chakula maalumu (special diet) kwa wagonjwa wenye uhitaji huo. 

Utaratibu wa chakula cha mzabuni kwa wagonjwa
 Kuhusu utaratibu huo Bw. Aligaesha amesema Mzabuni ndiye atakayepika chakula kwa wagonjwa wote waliolazwa na atatayarisha, atakipeleka na kukikabidhi katika wodi husika ambapo jukumu la kumpa mgonjwa kifungua kinywa, chakula cha mchana na jioni linabaki wa Hospitali.
  
   Amesema wagonjwa watapatiwa milo mitatu kwa siku yaani asubuhi, mchana na jioni kazi itakayofanywa na muuguzi wa zamu ambaye atahakikisha wagonjwa wote wamepata chakula kufuatana na mahitaji (diet list) iliyowasilishwa jikoni kutokana na mahitaji yao ya kiafya.

Muda wa kuona wagonjwa
Kutokana na uamuzi huu, utaratibu wa ndugu kuleta chakula kwa wagonjwa waliolazwa wakati wa mchana umefutwa na hivyo mchana hatutakuwa na nafasi ya ndugu kuja kutembelea wagonjwa. Muda wa kutembelea wagonjwa utakuwa asubuhi saa 12 hadi saa moja kamili na saa 10:00 jioni hadi saa 12:00jioni ndipo ndugu wataruhusiwa kuingia ndani kuwaona ndugu zao waliolazwa. Katika muda huo ndugu ataruhusiwa kuja na chakula chochote anachofikiri atamuongezea mgonjwa wake kama matunda n.k

Uchangiaji huduma ya chakula
  Bw. Aligaesha amesema mgonjwa aliyelazwa atachangia kiasi cha shilingi 50,000 atakapolazwa ambapo kati ya hizo, shilingi elfu 10,000 itakuwa ni gharama ya kumuona daktari (Consultation), shilingi elfu 10,000 ikiwa ni gharama ya kulazwa na bei ya chakula itakuwa shilingi elfu 30,000 sawa na shilingi elfu 6,000 kwa siku. Wastani wa mgonjwa kukaa wodini ni siku tano. Gharama hizo zinahusika kwa muda wote atakaokuwa amelazwa.

Kwa sasa Hospitali inatoa chakula kwa wagonjwa 650 ambao wamepata rufaa kutoka hospitali za nje ya mkoa wa Dar es Salaam kwa gharama wastani wa shilingi 1.8 bilioni kwa mwaka, sawa na shilingi 150 milioni kwa mwezi kwa vyakula pamoja na  gharama nyingine kama vile za nishati. Takribani wagonjwa kati ya 600 na 700 ambao rufaa zao ni kutoka Hospitali za Dar es Salaam walikuwa hawapati chakula kutoka Hospitalini, na ilibidi ndugu zao wawaletee chakula. Hata hivyo, Hospitali ilikuwa inawapatia chakula tu kama ndugu zao wakishindwa kufanya hivyo.

  Hitimisho.
“Uongozi wa Hospitali unaamini kwamba mabadiliko haya hayatamuongezea mgonjwa gharama, bali yatampunguzia gharama pamoja na ile adha kama ilivyoainishwa hapo juu. Aidha, uongozi unaamini kwamba uamuzi huu unaendana na azma nzima ya kuboresha utoaji huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuboresha mazingira ya Hospitali. Tunaomba ushirikiano wenu katika kutekeleza jukumu hili ili kusudi wagonjwa waweze kuhudumiwa vizuri zaidi” amesisitiza Bw. Aligaesha.

No comments: