Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Tamasha Fadhili Mtoto Asome pamoja na Binti Clubs iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Binti Foundation ambapo aliahidi kuwasomesha watoto 100 na aliwasihi Wanawake wanapoweka mipango ya kimaendeleo kuwashirikisha pia wanaume.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwa pamoja na mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa mara baada ya uzinduzi wa Binti Clubs jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya watu waliojitokeza kwenye Tamasha Fadhili Mtoto Asome pamoja na Binti Clubs iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Binti Foundation ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan akipitia kitabu cha Binti Foundation wakati wa Tamasha Fadhili Mtoto Asome.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akitazama jambo liliokuwa linaendelea (halionekani pichani) pamoja na Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa Binti Foundation Johari Sadiq .
Sehemu ya watoto walioshiriki kuonyesha mitindo mbali mbali ya Mavazi pamoja na Wabunifu wao.
Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameyataka Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini (NGOs) yanayoshughulikia masuala ya wanawake na watoto kujenga utamaduni wa kushirikisha wanaume katika kampeni za kumwinua mtoto wa kike kwa lengo la kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.
Mheshimiwa Samia ametoa kauli hiyo jana kwenye hafla ya uzinduzi wa Binti club iliyofanyika sambamba na harambee ya fadhili mtoto asome ya kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto 500 wa wilaya ya Kinondoni iliyoandaliwa na Shirika lisislo la Kiserikali la Binti Foundation katika ukumbi wa PSPF jijini Dar es salaam
Alisema wanaume kama wakala wa mabadiliko wanapaswa kushirikishwa na wajue ajenda ili wawe mabalozi wazuri katika kuzungumzia umuhimu wa kumwinua mtoto wa kike kielimu, kiafya na kwenye masuala ya ujasiriamali.
"Tuwaingize wanaume kama wakala wa mabadiliko, tuwashirikishe, wajue ajenda zetu katika mapambano hayo. wanaume wanashikilia sehemu nyingi, watumie nafasi hizo tulete mabadiliko," alisema Makamu wa Rais na kuongeza."Penye mkusanyiko wa watu 100, ukiingiza wanaume 20, na wakajua madhumuni ya mkusanyiko wetu, wataenda kushawishi wenzao 20,000 huko nje."
Aliipongeza Taasisi hiyo ya Binti Foundation kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika suala la elimu kwani safari ya mtoto wa kike ya kupata elimu inakuwa na ugumu zaidi kuliko wanaume kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mila potofu, hali ya uchumi katika familia na jinsi jamii inavyomwangalia kutokana na ujanajike wake.
"Tuna kazi kubwa ya kumtayarisha mtoto wa kike aweze kupambana na changamoto zinazomzunguka," alidokeza.
Mheshimiwa Samia alitumia fursa hiyo kuelezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na changamoto za elimu ikiwa ni pamoja na kuondoa ada katika shule za msingi na sekondari, kuboresha ajira za walimu pamoja na maslahi yao, kujenga mabweni kwa wasichana na kuondoa tatizo la madawati ambapo amewashukuru Watanzania kwa kuchangia madawati.Aliwataka wazazi kuwatunza watoto wao kwani ni zawadi kutoka kwa Mungu na kuhakikisha wanapata elimu zote ya dini na ya dunia ili kuwajenga kimaadili waweze kuwa raia wema.
Mtendaji Mkuu wa Binti Foundation Johari Sadik alimweleza Makamu wa Rais kuwa shirika hilo liliamua kuunga mkono jitihada za serikali ili kuwawezesha watoto kumudu masomo yao na hatimaye kufikia malengo yao."Kwa hiyo ukiwa na fedha taslimu, ama vifaa kama vile kalamu, madaftari, pedi, vyote tunapokea kwa ajili ya kusaidia watoto ambao malengo yao yanaweza yasitimie kutokana na changamoto hizo,"
Kampeni hiyo ya fadhili mtoto asome imeanzia kwa watoto 500 wanaoishi kwenye mazingira magumu wa shule za msingi Mwananyamala, Hananasif, Kumbukumbu na Msasani zilizoko katika wilaya ya Kinondoni, mkoa wa Dar es salaam.Katika hafla hiyo iliyopambwa na onesho la mavazi la watoto Makamu wa Rais ambaye alikubali kuwa mlezi wa Binti Foundation aliahidi kusomesha watoto 100 wakati mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa alitoa ahadi pia ya kusomesha watoto 50.
Comments