Thursday, June 30, 2016

KONGAMANO LA KUBADILISHANA UZOEFU WA MAFUNZO YA TAALUMA UFARANSA NA TANZANIA LAFANYIKA


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (katikati) akisalimiana na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kulia) alipowasili katika ofisi za ESRF jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak.
(Picha na Modewjiblog)
 
Taasisi ya utoaji mafunzo ya Ufaransa ya AFPA ndiyo ilikuwa inaendesha mafunzo hayo wakibadilishana uzoefu na wadau wa Tanzania kutoka sekta binafsi.
Akifafanua zaidi Dkt. Kida alisema kwamba kongamano hilo limelenga zaidi katika kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto zinazojitokeza na fursa zilizopo katika mafunzo, ukuzaji na uendelezaji taaluma.
Dkt. Kida alifurahishwa na mchanganyiko wa watu kutoka sekta binafsi waliofika katika kongamano hilo ambao aliamini kwamba wataelezea uzoefu wao katika kukabiliana na changamoto za taaluma katika makampuni yao.
Aidha alisema kwamba wadau hao wa Tanzania watapata uzoefu wa timu ya wataalamu wanne kutoka kwa wakala wa mafunzo ya taaluma nchini Ufaransa (AFPA) ambao wataeleza miaka 60 ya uzoefu katika masuala ya mafunzo ya taaluma na uendelezaji wa utaalamu.
 Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak (kushoto) akibadilishana mawazo na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida katika ofisi za ESRF jijini Dar es Salaam.
 
Alisema anaamini kwamba mchanganyiko huo wa wadau utasaidia katika kukabiliana na tatizo la taaluma katika soko la ajira la Tanzania.
Alisema mazungumzo hayo ni muhimu sana katika kuibua fursa hasa wakati taifa hili linajipanga kuelekea katika uchumi wa kati wa viwanda na bila wataalamu wenye taaluma zao makamapuni na viwanda vingi vitakuwa na shida kubwa.
Alisema changamoto kubwa inayokabili taifa la Tanzania kuelekea nchi ya viwanda kama ilivyo katika nchi nyingine zinazoendelea ni ukosefu wa taaluma na utaalamu.
“Ukosefu wa wafanyakazi wenye taaluma katika ngazi zote ni tatizo kubwa linalokabili harakati za kuelekea uchumi wa viwanda” alisema Dkt. Kida.
Anasema pamoja na matatizo hayo taasisi yake tayari imeshaanza kushughulikia shida hiyo ya taaluma nchini Tanzania kwa kuwa na makongamano mbalimbali makubwa yanayokutanisha wadau kuzungumzia hali hiyo.
Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak (kulia) akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero (kushoto) alipowasili ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (katikati) kabla ya kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano.
 
Alisema kwa mfano mwaka 2015 iliendesha jukwaa la mafunzo ya ufundi (VTEC) Africa. Katika jukwaa hilo lililofanyika Machi 10 -12 mwaka huo walizungumzia mafunzo ya utaalamu wa gesi na mafuta kwa mataifa ya Afrika. Jukwaa hilo liliendeshwa kwa kushirikiana na kampuni ya Uingereza ya Getenergy.
Aidha Oktoba 9, 2015 iliendesha semina kuhusu uumbaji wa programu za mafunzo kwa aili ya kupata wataalamu wa gesi na mafuta.
Lakini, alisema, kuanzia Julai 2014, ESRF imekuwa ikishirikiana na shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kutekeleza mpango wa miaka mitano wa mafunzo ya kinadharia na utaalamu yenye mfumo wa Ushiriki ambapo ESRF yenyewe hutoa msaada wa kitawala na lojistiki kwa wanafunzi ili waweze kwenda kuhudhuria mafunzo nje ya nchi.
Aidha ESRF imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali na uchambuzi kuhusiana na uendelezaji wa taaluma nchini Tanzania na moja ya ya tafiti hiyo ni kudorora kwa ubora wa elimu Tanzania na namna ya kuzuia anguko hilo na kulibadili.
Mwaka 2014 na mwaka huu kuna mada inayozungumzia uendelezaji wa mafunzo ya taaluma na uwezo wa uzalishaji Tanzania.Mada hii ni sehemu ya taarifa ambazo zitapatikaa katika ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2017.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kulia) akiongozana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano wa ESRF. Nyuma ni Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak akibadilishana mawazo na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi pamoja na Mkurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Ally Msaki.
KONGAMANO kubwa la aina yake limefanyika mjini Dar es salaam ambapo washiriki walizungumzia namna ya kuendeleza rasilimali watu katika eneo la utaalamu na taaluma katika shughuli mbalimbali za uendelezaji wa makampuni na viwanda.
Kongamano hilo ambalo lilihudhuria na watu wenye kariba kubwa katika masuala ya viwanda na biashara akiwemo Dkt. Reginald Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa makampuni ya IPP na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF);na Balozi wa Ufaransa nchini Malika Berak liliangalia uhaba wa wataalamu na namna ya kuuondoa uhaba huo wakati taifa linaelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
Wengine waliokuwepo katika kongamano hilo Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero na maofisa wa serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akikaribisha washiriki na wadau wengine alisema kwamba mafunzo hayo yaliyoratibiwa kwa pamoja katika wataalamu wa Ufaransa, ESRF na Benki ya Maendeleo ya Afrika yamelenga kudadavua tatizo lililopo na kulipatia ufumbuzi.

No comments: