*Nyang’hwale, Geita*
Wachimbaji wadogo wa madini wilayani Nyang'hwale, mkoani Geita, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye maeneo ya migodi, hatua inayopunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija katika shughuli za uchimbaji.
Shukrani hizo zimetolewa wakati Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alipozindua mradi wa kuzalisha nishati ya umeme wenye uwezo wa KVA 500 kwenye Mgodi wa wachimbaji wadogo katika eneo la Igalula, wilayani Nyang'hwale. Mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 426 na ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya nishati katika maeneo ya uchimbaji wa madini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Mavunde amesema Serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na uzalishaji katika sekta ya madini kwa kusambaza umeme kwenye migodi ya wachimbaji wadogo na wa kati.
Amesema Serikali tayari imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 7 kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya migodi nchini, hatua iliyowezesha wachimbaji kupunguza utegemezi wa mitambo inayotumia mafuta na hivyo kushusha gharama za uzalishaji huku ikiongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji.
Katika kuendelea na ziara yake, Waziri Mavunde amekagua mradi wa maji safi na salama unaotekelezwa katika Kijiji cha Kakola, ambao unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wananchi 24,801
Amesema mradi huo unatekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi, hususan wanawake, wanaondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
"Ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani inaendelea kutekelezwa kwa vitendo kupitia miradi ya maji kama huu wa Kakola ambao utaboresha afya, ustawi na shughuli za kiuchumi za wananchi," amesema.
Katika sekta ya elimu, Waziri Mavunde amezindua Shule ya Msingi Imara Baruti iliyojengwa ili kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa takribani kilomita nne kwenda kusoma katika Shule ya Msingi Shabaka.
Amesema ujenzi wa shule hiyo unatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayosisitiza ujenzi wa shule karibu na makazi ya wananchi ili watoto wapate elimu katika mazingira bora.
"Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuthibitisha kuwa ahadi zinazotolewa kwa wananchi si maneno ya kampeni pekee, bali ni mipango inayotekelezwa kwa vitendo kwa manufaa ya Watanzania," amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, amempongeza Waziri Mavunde kwa kufanya ziara ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo mkoani humo, akisema hatua hiyo imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuimarisha ufuatiliaji wa huduma zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
Shigella amebainisha kuwa uwekezaji unaoendelea katika sekta za madini, elimu, maji na nishati unaendelea kuifanya Geita kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa madini na maendeleo ya kijamii nchini.







No comments:
Post a Comment