Wednesday, June 15, 2016

TAASISI ZA FEDHA ZASHAURIWA KUPITIA UPYA RIBA INAZOTOZA KWENYE MIKOPO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akihutubia wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi kutoka mikoa yote nchini (hawapo pichani), katika ukumbi wa Mikutano wa Kambarage ulioko katika Jengo la Hazina Mjini Dodoma Wadau wa sekta ya Benki za Wananchi kutoka mkoani Mwanza, wakisikiliza kwa makini mada zilizotolewa kuhusu uanzishwaji wa benki hizo nchini, katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Kambarage ulioko katika Jengo la Hazina mjini Dodoma

Wakiri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Benki za wananchi nchini, Bi. Elizabeth Makwabe, baada ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano huo uliowashirikisha viongozi wa mikoa mbalimbali nchini katika ukumbi wa Kambarage, Jengo la Hazina mjini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, (Kushoto) akibadilishana mawazo na Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa siku moja wa wadau wa Jumuiya ya Benki za wananchi, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kambarage, ulioko katika jengo la Hazina Mjini Dodoma.Picha zote na Benny Mwaipaja, WFP


Na Benny Mwaipaja-WFP

WAZIRI MKUU, Mhe. Kassim Majaliwa, amezishauri taasisi za fedha nchini zipunguze viwango vya riba zinazotoza kwenye mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hususan waishio vijijini kujikwamua kiuchumi

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Juni 15, 2016, wakati akifungua mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi (COBAT), ulioshirikisha viongozi wa mikoa 28 nchini, uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hazina Mjini Dodoma.

Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema kuwa riba kubwa inayotozwa na taasisi hizo za fedha ni kubwa na kuwafanya wananchi wengi washindwe kunufaika na fursa za mikopo inayotolewa, hali inayowafanya waendelee kuwa masikini.

“Kama Benki zitatoa mikopo yenye riba nafuu, kila mwananchi atamudu kupata mtaji na kufanya biashara yake akijua kuwa riba si kubwa na tayari Serikali imeanza kufanya mazungumzo na taasisi za fedha kuhusu jambo hili ili ziweze kufanya mapitio ya riba zake”Aliongeza Mhe. Kassim Majaliwa

Ameipa mikoa ambayo haijaanzisha benki za wananchi-COBAT, muda wa miezi mitatu kuanzisha mchakato huo ili kufikisha huduma rasmi za kifedha kupitia benki hizo ili kuchochea na kuamsha uzalishaji mali wenye tija katika jamii.

Amesema lengo muhimu la kuwainua wananchi kimaisha litatimia kwa kuhamasisha wananchi mijini na vijijini, wenye kipato cha chini kabisa katika kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba na kuwekeza katika hisa ili kukuza mitaji itakayosaidia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao yote.

Ameahidi kuwa Serikali itaangalia uwezekano wa kuiwezesha mikoa itakayoonesha ari zaidi ya kuanzisha benki zao za wananchi kwa kuzishirikisha Halmashauri za wilaya, Manispaa, Miji na Majiji.

“Inawezekana kabisa kuanzisha benki hizo kwa kukusanya hisa kutoka kwa wananchi na Halmashauri zikachangia ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kufikiwa na huduma za kibenki katika maeneo yao”Alisisitiza Waziri Mkuu.

Amesema ni matumani ya serikali ya awamu ya tano kwamba uanzishwaji wa benki hizo una umuhimu mkubwa kwa kuwa zitakuwa kiunganishi mahsusi ambacho kikiwa imara kitaleta mabadiliko chanya katika kuwawezesha wananchi kujikwamua na kujiletea maendeleo ya haraka.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2016, mikoa 8 tu ya Tanzania bara ndiyo imeanzisha benki za wananchi-COBAT kati ya mikoa 26 iliyopo.

Amezitaja benki hizo zilizoko chini ya Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania-COBAT kuwa ni Mucoba (Mufundi), Mbinga (Mbinga), Mwanga (Mwanga), Uchumi (Moshi), Tandahimba (Mtwara), Meru (Arusha), Njombe (Njombe) na Efatha (Dar es salaam)

Dkt. Mpango amesema kuwa Benki hizo zinawateja wanaokadiriwa kufikia 600,000 zikiwa na jumla ya mali iliyofikia shilingi Bilioni 86.3 na amana za wateja shilingi Bilioni 69.2 na kutoa mikopo kwa wateja wake inayofikia shilingi Bilioni 56.2

“Mpango wa kuhakikisha huduma za fedha zinawafikia wananchi wengi zaidi ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya taifa inayolenga kuipeleka Tanzania katika nchi ya kipato cha kati na yenye uchumi imara ifikapo mwaka 2015” Amesisitiza Dkt. Mpango

Amesema hadi kufikia Desemba mwaka 2015, Taasisi za benki za wananchi za mikoa, vyama vya ushirika vya akiba na mikopo, zimeongezeka hadi kufikia 4,093, zikiwa na wanachama 733,876 na kuwekeza kiasi cha shilingi Bilioni 377.6

“Aidha, Asasi za Fedha za Kijamii (Vicoba, Vsla, Rosca), zinakadiriwa kufikia 100,000 na zina wanachama milioni 2.2 na mtaji wa shilingi Trilioni 1.2” aliongeza Dkt Mpango

Amesema kuwa utafiti uliofanyika hivi karibuni na shirika la Finscope umebaini kuwa asilimia 57.4 ya watanzania wanapata huduma rasmi za kifedha, ambapo kati ya hao, asilimia 13.9 wanapata huduma za kibenki huku asilimia 43.5 wanapata huduma za kifedha zisizo za kibenki.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amezitaja changamoto zinazoikabili sekta ya Fedha nchini kuwa ni upungufu wa mitaji, ukusanyaji mdogo wa amana, kiwango cha riba kuwa juu, ushindani kutoka benki za biashara na taasisi zingine za Fedha, kukosekana kwa wataalamu wa kuziendesha na kukosekana kwa sheria na kanuni mahsusi kwa benki za wananchi na Ushirika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania-COBAT, Elizabeth Makwabe, amesema kuwa katika kipindi cha miaka 20 sasa, benki za wananchi zimeendelea kupanua huduma zake ambapo hadi sasa, mali, amana na mikopo vimeongezeka kutoka shilingi Bilioni 71.2 mwaka 2014 hadi kufikia shilingi Bilioni 86.3 mwaka 2015

Ameiomba serikali kuwekeza fedha za kutosha kwenye benki za wananchi katika mfumo wa fedha za kuzungusha (Revolving Fund) ili kusisimua uchumi katika maeneo ya vijijini pamoja na kuzitaka Halmashauri za wilaya kuwekeza mitaji kwenye benki hizo katika maeneo yao.

Akitoa neno la Shukrani kwaniaba ya wakuu wa mikoa waliohudhuria mkutano huo, mkuu wa mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera, ameahidi kuwa mikoa yote 18 ambayo haijaanzisha benki za wananchi itahamasisha na kuanzisha benki hizo kwa faida ya wananchi wao.

No comments: