RAIS MAGUFULI AFANYA UTEUZI WA WAKUU WA WILAYA NA AFANYA MABADILIKO MADOGO YA WAKUU WA MIKOA




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Juni, 2016 amefanya mabadiliko madogo katika safu ya wakuu wa mikoa na amewateua wakuu wa wilaya 139.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema katika mabadiliko hayo Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Bi. Zainab R. Telack kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Bi. Zainab R. Telack anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Anna Kilango Malecela ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Rais Magufuli pia amemteua Dkt. Binilith Satano Mahenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Dkt. Binilith Satano Mahenge anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Said Thabit Mwambungu ambaye amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es salaam ambako atapangiwa majukumu mengine.

Aidha, Rais Magufuli amemteua Dkt. Charles F. Mlingwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Dkt. Charles F. Mlingwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Stanslaus Magesa Mulongo ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Wakuu wapya wa mikoa walioteuliwa wataapishwa tarehe 29 Juni, 2016 saa tatu kamili asubuhi Ikulu Jijini Dar es salaam na mara baada ya kuapishwa watakula kiapo cha maadili ya uongozi.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Juni, 2016 amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 139.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema katika uteuzi huo Rais Magufuli amezingatia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na umri ambapo kwa wale ambao umri wao ni zaidi ya miaka 60 ameamua wastaafu.

Mhe. Rais amewashukuru sana kwa utumishi wao mzuri na amesema pale ambapo itahitajika, serikali itaendelea kuwatumia katika majukumu mengine.

Katika uteuzi huo, Wakuu wa Wilaya waliopo sasa ambao wamebaki katika nafasi zao ni 39. Pia Rais Magufuli amewateua Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri 22 kuwa Wakuu wa Wilaya kutokana na utendaji wao mzuri.

Aidha, nafasi 78 za uteuzi wa Wakuu wa wilaya zimejazwa na watanzania wengine ambao wameteuliwa kwa mara ya kwanza wengi wao wakiwa ni vijana, wenye elimu ya kutosha na uzoefu katika maeneo mbalimbali.

Walioteuliwa kuwa wakuu wa wilaya ni kama ifuatavyo (Orodha imepangwa kulingana na mikoa).

Comments