Wednesday, June 29, 2016

VIWANDA VISIVYO ENDELEZWA KURUDISHWA KWA WATANZANIA


Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali ambavyo haviendelezwi kutwaliwa ili kutolewa kwa wawekezaji wenye uwezo wa kuviendesha.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Mwakasaka aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa juu ya mwekezaji wa kiwanda cha nyuzi Tabora kwa kushindwa kuendeleza kiwanda hicho.

“Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na tathmini ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa na Serikali kikiwemo kiwanda cha nyuzi cha Tabora ili kujiridhisha kama wawekezaji wa viwanda hivyo wanatimiza matakwa ya mkataba na Serikali,” alifafanua Mhe. Mwijage.
Aliendelea kwa kusema kuwa, ikiwa viwanda hivyo vitabainika kubadilishwa matumizi yake au kutoendelezwa basi Serikali itavirudisha kwa watanzani ili viweze kuendelezwa.
Aidha Mhe. Mwijage amesema kuwa, kwa sasa mwitikio wa kuviendeleza viwanda ambavyo vilikuwa havizalishi ni mzuri kwani viwanda vingi vimeanza kufanya kazi lakini kwa wale ambao watashindwa kabisa  kuviendeleza basi viwanda hivyo vitarejeshwa kwa watanzania.
Vile vile Mhe. Mwijage amesema kuwa dhana ya Serikali ya awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda inaenda pamoja na kurejesha Serikalini viwanda vyote vilivyobinafsishwa lakini haviendelezwi ili vitolewe kwa wawekezaji wengine.
Sambamba na hayo Mhe. Mwijage amesema kuwa kufufua viwanda, hasa viwanda vya nguo ni pamoja na wakulima wa pamba kulima zao hilo kwa wingi kwa ajili ya uchakataji pamoja na kudhoofisha uingizaji wa nguo za mitumba nchini.
Wizara hiyo inaendelea na kushawishi wawekezaji mbalimbali ili kujenga viwanda vingi iwezekavyo kwa ajili ya uchakataji wa mazao yanayolimwa nchini pamoja na mifugo

No comments: