Wednesday, September 17, 2014

UNCDF KUENDELEA KUSAIDIA KUJENGA UWEZO WA KIFEDHA KUHUDUMIA MAENDELEO

DSC_0053
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu kataka Wizara hiyo Dkt. Deogratius Mtasiwa, akizungumza kwenye mkutano wa watendaji waandamizi wa serikali kutoka katika Ofisi ya WaziriMkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) pamoja na waandishi wa habari kuhusiana na Programu ya Utafutaji Fedha Nchini kwa maendeleo ya wananchi (Global Local Finance Initiative (LFI) ambayo ilianza katika awamu ya majaribio 2012 na kuonyesha mafanikio. Kulia ni Mshauri Mkuu wa Ufundi wa programu hiyo nchini Tanzania , Peter Malika.
Na Mwandishi wetu
Mfuko wa Mtaji wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, (UNCDF) umefurahishwa na programu zinazoendeshwa nchini kwa msaada wake na kusema upo tayari kuendelea kufanyakazi na serikali na wananchi wa Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa katika ziara ya Katibu Mtendaji wa UNCDF, Judith Karl, ambaye anaitembelea Tanzania kwenye mkutano wake na watendaji waandamizi wa serikali kutoka katika Ofisi ya WaziriMkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) jana.
Karl ambaye ameongozana na Mkurugenzi wa Local Development Finance kutoka Makao Makuu ya UNCDF, New York, David Jackson alisema wamefurahishwa namna Tanzania inavyotekeleza mpango huo wa kuwezesha watanzania kuchangia miradi yao ya maendeleo kwa kutumia vyanzo vya ndani katika halmashauri mbalimbali.Miongoni mwa halmashauri zilizofanya vyema ni Same na Kibaha.
Akiwa na Mshauri Mkuu wa Ufundi wa programu hiyo nchini Tanzania , Peter Malika, Mtendaji huyo alisema wamefika kutia saini mkataba wa maelewano kati ya Tanzania na shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutekeleza miradi 25 na hasa baada ya awamu ya kwanza wa miradi mitano kuonesha mafanikio makubwa.
Akizungumza Karl pamoja na kuelezea kazi za UNCDF nchini Tanzania alitangaza kuanzishwa kwa Programu ya Utafutaji Fedha Nchini kwa maendeleo ya wananchi (Global Local Finance Initiative (LFI) kwa mwaka 2014-2017, ikiwa ni jitihada mpya ya UNCDF iliyoanzishwa kufuatia maarifa yaliyopatikana katika utekelezaji wa LFI ya kwanza (Tanzania) katika awamu ya majaribio (2012-2015).
DSC_0178
Katibu Mtendaji mpya wa Mfuko wa Mtaji wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), Bi Judith Karl akizungumza na baadhi ya wajumbe wa TAMISEMI pamoja na waandishi wa habari juu Programu ya utafutaji fedha nchini kwa maendeleo ya wananchi (Global Local Finance Initiative (LFI), ambapo alitangaza kuizindua rasmi program hiyo katika mkutano uliofanyika kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu – OWM-TAMISEMI, Dkt. Deogratius Mtasiwa.
Hadi sasa, programu ya majaribio ya LFI nchini Tanzania inasaidia miradi 25 ya miundombinu iliyoanzishwa na wawekezaji wa umma na binafsi na ambayo iko katika hatua mbalimbali za uendelezaji. Lengo la programu hiyo ni kuanzisha makampuni makubwa ya uwekezaji katika halmashauri ili kupunguza mchango wa serikali kuu katika mambo ambayo yanaweza kufanywa na wananchi na wao wakabaki katika sera na mipango mikubwa.
Miradi imetawanyika katika sekta mbalimbali zikiwezo za usindikaji bidhaa za kilimo, nishati, miundombinu ya utoaji huduma za jamii, mawasiliano, na uzalishaji viwandani, katika mikoa 10 kote nchini.
Miradi mitano iliyopiga hatua kubwa zaidi inatarajiwa kufikia kikomo cha bajeti yake katika miezi sita hadi tisa ijayo ambapo dola milioni 26 za mtaji wa ndani katika muundo wa mkopo na misaada ipatayo dola milioni 3 ilihamasishwa.
Msaada wa LFI kwa miradi ambayo iko katika muundo wa utaalamu wa kiufundi, kutoa amana, misaada ya kifedha , mikopo ambayo inahitajika sana kwa miradi midogo na ya kati ya miundombinu ili ivutie uwekezaji.
Matokeo ya jumla ya LFI ni kuongezeka kwa ufanisi wa rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi ya hapa nchini kupitia uhamasishaji kwanza kabisa wa mtaji binafsi kutoka nchini na masoko ya mitaji ilikuwezesha na kuhamasisha maendeleo ya mahali yaliyojumuishi na endelevu.

No comments: