Monday, February 17, 2014

Felix Ngamlagosi ateuliwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)

Felix Ngamlagosi 
Aliyekua  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)Bw. Haruna Masebu,ambaye amemaliza  muda wake tarehe 31 Desemba 2013, baada ya kuitumikia Mamlaka kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja kwa mujibu wa Sheria ya EWURA.
-- 
 
Taarifa inatolewa kwa umma kwamba, kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha Sheria namba 14(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, Sura Na. 414, Waziri wa Maji, Mhe., Prof., Jumanne Maghembe (MB), ambaye pia ni Waziri anayehusika na EWURA, amemteua Bw. Felix Ngamlagosi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kuanzia tarehe 1 Februari 2014.

Bw. Ngamlagosi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Haruna Masebu, aliyemaliza muda wake tarehe 31 Desemba 2013, baada ya kuitumikia Mamlaka kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja kwa mujibu wa Sheria ya EWURA. 

Kabla ya uteuzi wake, Bw. Ngamlagosi alikuwa Mkurugenzi wa Udhibiti wa Kiuchumi wa EWURA, nafasi aliyoitumikia kwa miaka saba.

Bw. Ngamlagosi ana Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uchumi, kutoka Moscow Finance Academy, Urusi, (1990 – 1996); Stashahada ya Uandaaji Sera na Miradi ya Maendeleo kutoka Institute of Social Studies (ISS), The Hague – Netherlands (year 2000); Fundi Mchundo kutoka Chuo cha Maji (1984 – 1987); na Tuzo ya Uzamili Bingwa kwenye Udhibiti wa Huduma za Kiuchumi iliyotolewa kwa pamoja kati ya Taasisi ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi ya Washington, Marekani, na Kituo cha Maji, Uhandisi na Maendeleo cha Chuo Kikuu cha Loughborough (WEDC/LU) cha Uingereza (2013).

Ni mtaalam wa masuala ya udhibiti wa huduma za nishati na maji, akiwa amebobea kwenye uchambuzi wa bei za huduma, ufuatiliaji wa taasisi zinazotoa huduma, mbinu za kulinda maslahi ya watumiaji, na uandaaji wa mifumo ya mawasiliano na wadau katika sekta za umeme, petroli, gesi asili na maji. 

Kabla ya kujiunga na EWURA, Bw. Ngamlagosi alifanya kazi Wizara ya Maji, Nishati na Madini na baadaye Wizara ya Maji kwa jumla ya miaka 17 akipanda vyeo mbalimbali hadi kuwa Mchumi Mwandamizi. 

Pia alichangia kazi za kitafiti, kama mtaalam-mwenza, za Uchambuzi wa Matumizi ya Fedha za Umma kwenye Sekta ya Maji zilizofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) mwaka 2001 na 2002, pia na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 2003 – 2005. 

Akiwa mwenye uzoefu mkubwa kwenye sekta zinazodhibitiwa na EWURA, Bw. Ngamlagosi anategemewa kutekeleza majukumu na wajibu wake kama Mkurugenzi Mkuu wa EWURA kwa uaminifu na weledi wa hali ya juu. 

Kwa maelezo hayo, nachukua fursa hii kuwataarifu wadau wetu, watoa huduma na umma kwa ujumla kuhusu mabadiliko hayo. Pia, mnaombwa kumpa Bw. Ngamlagosi ushirikiano ili kumuwezesha kutekeleza kikamilifu majukumu yake kama Mkurugenzi Mkuu wa EWURA.
Imetolewa na:
 

 
Simon F. Sayore,
 
Mwenyekiti,
 
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji
 
Februari 14, 2014.

No comments: