Friday, February 14, 2014

TRA YASIKITISHWA NA MGOMO WA WAFANYABIASHARA KWA KUFUNGA MADUKA MAENEO MBALIMBALI NCHINI



Mamlaka ya Mapato Tanzania inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania na wafanyabiashara kwa ujumla Kuwa inasikitishwa  na mgomo wa wafanyabishara kwa kufunga maduka maeneo mbali mbali nchini.
Ifahamike kuwa Matumizi ya mashine ya EFD ni jambo la kisheria  na lilipitishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2011.

Pamoja na sheria kupitishwa, viongozi wakuu wa nchi walikwisha litolea tamko kwa nyakati tofauti kwa kuanzia na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mwezi wa Machi 2011.

Pia Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohammed Gharib Billal alikazia jambo hili tarehe 8 Mwezi November mwaka 2013.

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda alilitolea tamko pia Mwezi Desemba 2013  wakati akiahirisha Bunge kwa kusisitiza msimamo wa serikali kwa utekelezaji wa kisheria wa matumizi wa mashine za EFD.

Tarehe 29 Janauri 2014, Waziri wa Fedha Mhe Saada Mkuya Salum aliweka bayana msimamo wa Serikali kwa kusisitiza kuwa Matumizi ya mashine za EFD ni swala la kisheria na litaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa sheria akisisitiza kuwa muda wa mwisho wa nyongeza kwa wafanyabishara kununua mashine ilikuwa ni Tarehe 31 Januari 2014 baada ya kuongeza muda mara tatu kwa nyakati tofuati.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pia kwa nyakati tofauti na maeneo  tofuati imelitolea tamko jambo hili na itaendelea kufanya hivyo.

Kwa masuala ya kiutendaji yaliyolalamikiwa yamefanyiwa kazi na yanaendelea   kufanyiwa kazi ikiwemo utoaji wa Elimu kwa umma.

Mamlaka ya Mapato Tanzania  inapenda kuwafahamisha wafanyabiashara na umma kwa ujumla kuwa watu wanaolazimisha wafanyabishara wenzao kufunga maduka kwa kuwatishia na  kuwashurutisha wanavunja sheria kwa kusababisha uvunjifu wa amani nchini na hivyo mkono wa sheria utawafikia. Pia imefahamika kuwa baadhi ya watu wanaoshurutishwa kufunga biashara sio walengwa bali hutumika kuhalalisha azma ya wale wenye nia mbaya

TRA imekuwa ikipokea taarifa na maombi kutoka kwa baadhi ya wafanyabishara na wananchi wema wakiomba ulinzi ili wafungue maduka yao na kufanya biashara maana ndio ajira yao na mahali pakujipatia riziki ya kila siku.

Ifahamike kwamba wale wote wanaoshinikiza na kulazimisha wenzao kugoma wanavunja sheria kwa kuwalazimishwa wafanyabiashara kugomea agizo halali la kisheria hivyo kwa wale wote wanaotishiwa au kushurutiswa watoe taarifa kwa  kupiga simu namba zifuatazo 0786 800 000, 0713 800333, 0800 110016 au barua pepe info@tra.go.tz

“PAMOJA TUNAJENGA TAIFA LETU”

IMETOLEWA NA KAIMU KAMISHNA MKUU

MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA

No comments: