Saturday, April 30, 2016

TPDC yakanusha kufungua Akaunti za ESCROW katika Benki ya Stanbic


Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, linapenda kutoa taarifa sahihi juu ya taarifa ambazo zimekuwa zikiandikwa na vyombo mbalimbali vya habari, pamoja na mitandao ya kijamii kuhusu TPDC kufungua Akaunti za ESCROW katika Benki ya Stanbic.

Ni vyema ikaeleweka kwamba, Akaunti ya  ESCROW  ni Akaunti  maalumu inayoweza kufunguliwa  baina ya  Kampuni, Taasisi,  au Mashirika mbalimbali ya binafsi na yale ya umma kwa matumizi maalumu. Lengo la Akaunti ya ESCROW ni kuhifadhi fedha au kupitisha malipo kwa ajili ya shughuli maalum ikiwemo miradi au kazi yoyote maalumu na malipo haya hufanyika baada ya pande mbili kuridhia. 

TPDC ilifungua Akaunti tatu za Esrow baada ya Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT)  kutoa idhini kufunguliwa kwa akaunti kwenye Benki ya Stanbic, ikiwa ni moja ya masharti yaliyowekwa na mkopeshaji ili  kutoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya ya gesi asilia, kutoka Benki ya Exim ya China. Mkopeshaji alipendekeza Akaunti hizo zifunguliwe kwenye benki ya Stanbic na ambapo taratibu za manunuzi zilizingatiwa, ikiwemo ushindanishaji wa watoa huduma.

 Akaunti hizo tatu zilizofunguliwa ni pamoja na:
1. Akaunti ya Mapato ya Gesi 
Lengo la akaunti hii ni hifadhi mapato yote yatakayo tokana na mauzo ya gesi kwa njia ya bomba jipya.

2. Akaunti ya Uendeshaji 
Akaunti hii ina jukumu la kuhifadhi fedha zinazohitajika kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa mradi wa miundombinu hiyo mipya ya gesi asilia.

3. Akaunti ya Kulipia Deni
Akaunti hii imefunguliwa kwa ajili ya kulipa madeni yatokanayo na mkopo.

Akaunti hizi zinadhibitiwa na masharti yaliyowekwa kwenye makubaliano (Mkataba) ya Menejimenti ya Akaunti hizo yaliyosainiwa kati ya Benki ya Stanbic (kama Benki ), TPDC (kama mtumiaji wa mwisho), Benki ya Exim ya China (kama Wakopeshaji) na Wizara ya Fedha (kama mdeni kwa niaba ya Serikali ya Tanzania).

TPDC inapenda kuufahamisha umma kwamba, baada ya taratibu zote hizo kufuatwa, si sahihi kuuhusisha mchakato huu na tuhuma zozote na ukiukwaji wa sheria za nchi. Aidha, ifahamike kwamba Akaunti ya ESCROW ni akaunti ya kawaida kabisa katika utekelezaji wa miradi kama huu wa gesi asilia.

TPDC Kwa Maendeleo ya Taifa!
Imetolewa na:
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji- TPDC
S.L.P 2774
Dar Es Salaam

No comments: