Bw. James Oigo Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii NSSF akizungumza na waandhishi wa habari katika makao makuu ya shirika hilo jengo la Benjamin Mkapa wakati akielezea kuhusu waajiri wanaodaiwa madeni sugu ya michango ya wafanyakazi wao na kutamka kwamba wasipolipa michango hiyo mpaka ifikapo Juni 30 mwaka huu shirika hilo linawapeleka mahakamani, kulia ni mmoja wa maofisa waandamizi wa shirika hilo Bw. Salim Khalifan pamoja na maofisa wengine wa shirika hilo waliohudhuria katika mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia taarifa hiyo wakati Bw James Oigo Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii NSSF akizungumza nao katika mkutano huo.
………………………………………………………………………………………………………………………
Shirika la Taifa la Hifadhi ya jamii (NSSF) linapenda kutoa wito kwa waajiri wote wanaodaiwa malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wao kulipa malimbikizo hayo kabla ya tarehe 30.06.2016.
Waajiri ni moja kati ya wadau wakubwa wa shirika letu la NSSF kwa mujibu wa kifungu cha 11(6) na 12 (1) cha sheria ya NSSF, waajiriwa wana majukumu makubwa mawili.
- Kuhakikisha wafanyakazi wao wanaandikishwa katika shirika la taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF) mara tu wanapoajiriwa.
- Kuwakata michango yao asilimia 5% au 10% kutoka kwenye mshahara wa mwezi na kuwasilisha mchango huo ukiwa ni asilimia 20% ya mshahara wa mwezi, maana yake ni kwamba mwajiri baada ya kufanya makato kutoka katika mshahara wa mfanyakazi wake, anatakiwa kuongeza asilimia 10% au 15% ili ifikie asilimia 20% na kuwasilisha kwenye shirika.
Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha sheria ya NSSF no 28 ya mwaka 1997, waajiri wote wanatakiwa wawasilishe michango ya wafanyakazi wao ndani ya siku 30 toka tarehe ya mwisho wa mwezi husika, kwa mfano mchango wa mwezi machi,2016 , unatakiwa uwe umewasilishwa kwenye shirika kabla ya tarehe 30/4/2016 kinyume na hapo ni ukiukwaji wa sheria na ni kosa la jinai.
Lakini kuna baadhi ya waajiri kwa sababu wanazozijua wenyewe, wanashindwa kutekeleza hitaji hili la kisheria kikamilifu kwa kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati.
Kitendo cha kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati si tu kwamba ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 72 (d) cha sheria ya NSSF na ambayo adhabu yake ni pamoja na kifungo cha miaka 2 jela, lakini pia ucheleweshaji huu unasababisha madhara makubwa kwa wanachama na shirika kwa ujumla.
Comments