atumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (kulia) wakimlaki Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Jordan Rugimbana mara alipowasili ofisini.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana (kulia) akizungumza na Watumishi wa ofisi yake na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kumpokea Mkuu huyo ofisini.
Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo (hayupo pichani) na kufurahia jambo wakati wa hafla ya kumpokea Mkuu huyo ofisini.
Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo (hayupo pichani) na kufurahia jambo wakati wa hafla ya kumpokea Mkuu huyo ofisini.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa huo kuongeza bidii na ufanisi katika utoaji huduma na utendaji wa shughuli mbalimbali za serikali kwa kuzingatia sheria, Kanuni na taratibu za Nchi.
Vilevile, Rugimbana, pamoja na kuwasisitiza zaidi watumishi kuzingatia utii wa sheria, aliwataka wawe wawajibikaji ambapo alikemea vitendo kama majungu, dharau katika kazi, na kutokujituma kwa watumishi na kuwafananisha watumishi wazembe na majipu yanayohitaji kutumbuliwa.
Rugimbana aliyasema hayo mapema jana Aprili 4, 2016 wakati wa hafla ya kukaribishwa ofisini na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi hiyo ambapo wafanyakazi wote katika ofisi ya mkuu wa mkoa walishiriki.
”Tusiogopane bali tuheshimiane na kufanya kazi kwa ushirikiano Mkubwa ili kufanikisha lengo la kuleta maendeleo katika mkoa wetu wa Dodoma” alisisitiza Rugimbana.
Rugimbana pia aliwataka wananchi kuhakikisha watatekeleza maagizo ya Viongozi wa Serikali ya awamu ya tano kwa bidii akianzia na agizo la usafi wa mazingira alilolitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli ambapo aliagiza watumishi na wananchi wa Dodoma kujipanga kusafisha mji wa Dodoma kila mtu kwenye eneo lake na kutoa muda wa mwezi mmoja (1) wa kutekeleza agizo hilo.
Baada ya mwezi mmoja ameahidi ukaguzi wa usafi wa mazingira kwenye maeneo ya mji wa Dodoma utaanza ukihusisha usafi wa mazingira yote kwa ujumla, maeneo ya makazi, biashara, huduma mbalimbali, matumizi ya vyoo, ufyekaji nyasi maeneo yote ambapo alionesha kutofurahishwa na jinsi majani yalivyoota kiholela na kutengeneza vichaka maeneo mengi ya mji bila wahusika wake (wananchi na taasisi) kuyafyeka.
(Na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma)
Comments