DAWA NA VIFAA TIBA KUWA NJIANI MIAKA MINNE BOHARI YA DAWA (MSD) YATOA UFAFANUZI

 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu akionesha moja ya nyaraka inayoonesha upelekaji wa dawa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi kuhusu dawa za shilingi bilioni mbili kuwa njiani kutoka MSD Keko kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu mwaka 2012.
 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (kulia), akizungumza katika mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Victoria Elangwa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Sako Mwakalobo. 
 Ofisa Uhusiano Mkuu wa MSD, Etty Kusiluka (kulia), akizungumza katika mkutano huo wakati akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa MSD (kushoto), kuzungumza na wanahabari.Katikati ni Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Shughuli za Kanda, Terry Edward.

Na Dotto Mwaibale

BOHARI ya Dawa (MSD) imetoa ufafanuzi kuhusu dawa za sh.bilioni mbili kuwa njiani kutoka Bohari ya Dawa ya Keko kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu mwaka 2012.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema hakuna dawa ambazo ziko njiani tangu mwaka 2012 kutoka Bohari ya Dawa kwenda Muhimbili kama ilivyodaiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bungeni.

Bwanakunu alisema kuwa ripoti ya CAG ilionesha dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya sh.bilioni 2.03 havikuwa vimefika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu Mei 2012 licha ya kuonekana kwenye ankara 23 na Bohari ya Dawa.

"Tunapenda kutoa ufafanuzi kuwa ankara hizo sio kwamba dawa hazikufika hospitalini hapo, bali hazikuonekana kwenye vitabu vya kupokelea mali vya Hospitali ya Muhimbili" alisema Bwanakunu.

Alisema kwamba baada ya kupitia nyaraka zake, Bohari ya Dawa mpaka sasa imefanikiwa kupata uthibitisho wa hati za kupelekea mali za dawa na vifaa tiba vyote vilivyopokelewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambavyo ni pamoja na dawa za figo na moyo ambazo zilikwishapelekwa Muhimbili.

Aliongeza kuwa pamoja na juhudi za MSD imewasiliana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuainisha taarifa za kwenye ankara na shehena ya dawa na vifaa tiba vilivyopelekwa hospitalini hapo kwani utaratibu wa kupeleka na kukabidhi dawa hospitalini unamlazimu mpokeaji kusaini ankara ya kupeleka mali ambazo zote zipo MSD.

Akitolea ufafanuzi kuhusu picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii za gari aina ya lori lenye herufi "MSD" na kutoa maelezo kuwa ni gari la MSD amesema nembo inayoonekana kwenye gari hilo siyo ya Bohari ya Dawa.


Katika ripoti ya CAG ilionesha kwamba madawa na vifaa tiba ambavyo havikupokelewa kwa muda mrefu kutoka MSD vilikuwa vyenye thamani ya sh.bilioni 2.03 ambapo katika hali ya haikutajiwa kuchukua zaidi ya wiki moja kufikishwa sehemu husika ukizingatia ofisi zao ziko Dar es Salaam.

Comments