KESI YA KUPINGA MATOKEO YA UBUNGE JIMBO LA VUNJO,MREMA AKUBALI YAISHE ,AMTAMBUA MBATIA KAMA MBUNGE HALALI WA JIMBO LA VUNJO.


Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.
MBUNGE wa jimbo la Vunjo ,James Mbatia (TLP) ameshinda kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia chama cha Tanzania Labour (TLP)  Augustine  Lyatonga Mrema .
Mbatia ameshinda kesi hiyo baada ya upande wa mlalamikaji (Mrema) kuamua kufuta shauri hilo kwa hati maalumu iliyowasilishwa katika mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi huku akikiri kumtambua Mbatia kama mbunge halali wa jimbo hilo.
Mbali na utambuzi huo Mrema pia amekanusha maelezo pamoja na ushahidi wake aliowasilisha mahakamani hapo dhidi ya Mbatia,wananchi wa jimbo la Vunjo pamoja na taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini ambazo zilitajwa mahakamani hapo wakati wa ushahidi wake.
Ukiwasilisha hoja mahakamani hapo mbele ya Jaji wa mahakama kuu Lugano Mwandambo , upande wa mlalamikaji ukiongozwa na wakili January Mkobogho ulieleza kuwa pande mbili katika shauri hilo wamefikia makubaliano nje ya mahakama.
 Wakili Mkobogho aliiomba mahakama kuona makubaliano hayo ambayo yako katika maandishi kama alama kwa mujibu wa makubalinao waliyoafikiana baada ya kuingizwa na kupokelewa mahakamani hapo kama madai.
 Alisema kwa kuwa kesi hiyo ya uchaguzi ikiwa na maslahi mapana ya umma na kwa kuwa mlalamikiwa wa pili na watatu waliunganishwa kwenye shauri hili kwa mujibu wa sheria aliomba kila upande ubebe gharama zao.
Wakili Mkobogho alieleza kuwa kutokana na pande  zilizokuwa zinakwaruzana  wameamua kukaa na kumalizana wenyewe na kwamba haoni sababu za mlalamikiwa wa pili na watatu kutokubeba gharama zao wenyewe.
Jopo la mawakili sita wa upande wa utetezi ukiongozwa  na wakili , Mohamed Tibanyendera uliileza mahakama hiyo kwamba wanaungana na mtoa maombi kwa maslahi ya umma na kwamba wanakubali kila upande kubeba gharama zake.

Comments