Saturday, April 16, 2016

RAIS MAGUFULI AFUNGUA RASMI MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA JUU (FLY OVER) ENEO LA TAZARA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi na kuanza kwa ujenzi  wa mradi wa barabara ya juu Tazara Jijini Dar es Salaam. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akifungua  jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa barabara ya juu Tazara Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akifungua ramani ya mradi wa barabara ya juu eneo la Tazara kuashiria ufunguzi rasmi na kuanza kwa ujenzi  wa mradi huo Tazara Jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipokea maelekezo kuhusu mradi wa barabara za juu eneo la Tazara kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wakala wa barabara (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale katika ufunguzi rasmi wa mradi huo Jijini Dar es Salaam.


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbaliwa kitaifa na kimataifa wakati wa ufunguzi rasmi na kuanz akwa ujenzi  wa mradi wa barabara ya juu Tazara Jijini Dar es Salaam. 
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akihutubia katika hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya juu kwenye makutano ya barabara za Mandela na Nyerere maeneo ya Tazara Jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela, eneo la Tazara Jijini Dar es salaam ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2018.

Sherehe ya uzinduzi wa mradi huo imefanyika kando ya eneo la makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela Jijini Dar es salaam, ambapo pamoja na Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Mameya wa Jiji la Dar es salaam na Balozi wa Japan hapa nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida.

Barabara hiyo ya juu itakuwa ya kwanza kujengwa hapa nchini na ujenzi wake umepangwa kugharimu takribani shilingi Bilioni 100 ambapo kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 93.44 zitatolewa na Japan kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA), na Serikali ya Tanzania itatoa shilingi Bilioni 8.3.

Barabara ya juu itakayojengwa itakuwa na njia nne na urefu wa mita 300 kutokea maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es salaam kuelekea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, na inatarajiwa kupunguza kero ya msongamano wa magari yaendayo na yatokayo Uwanja wa ndege na Bandari ya Dar es salaam.

Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema barabara hiyo inajengwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya serikali yake ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari Jijini Dar es salaam, ambao kwa mwaka 2013 pekee utafiti umeonesha ulisababisha upotevu wa shilingi Bilioni 411.55

Rais Magufuli amebainisha juhudi nyingine za kukabiliana na msongamano wa magari Jijini Dar es salaam kuwa ni pamoja na kujenga barabara  ya njia sita ya Dar es salaam hadi Chalinze ambayo itakuwa na Flyover tano, ujenzi wa barabara nyingine za juu katika makutano ya barabara za Nelson Mandela, Morogoro na Sam Nojuma eneo la Ubungo na ujenzi wa daraja jipya la Salander lenye urefu wa kilometa 6.23 kuanzia Coco Beach hadi hospitali ya Agha Khan.

Juhudi nyingine ni ujenzi wa awamu ya pili wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika barabara za Kilwa, Chang'ombe na Kawawa, na ujenzi wa awamu ya tatu wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika barabara za Nyerere - Gongo la Mboto na Uhuru - Azikiwe.

Aidha, Rais Magufuli amezungumzia awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka, kuwa serikali yake imelazimika kusimamisha kuanza kwa huduma hiyo baada ya kubaini dosari katika mkataba wa mradi ambazo zingesababisha serikali kupoteza fedha nyingi na wananchi kutwishwa mzigo mzito wa viwango vikubwa vya nauli, na amewahakikishia wananchi wa Dar es salaam kuwa mabasi hayo yataanza kutoa huduma hivi karibuni baada ya kurekebisha kasoro zilizobainika.

Dkt. Magufuli pia amezungumzia usafi wa Jiji la Dar es salaam kwa kuwataka viongozi wa Manispaa zote za Jiji, kuhakikisha wanatafuta namna ya kudhibiti utupaji hovyo wa takataka ikiwemo kutoza faini kubwa kwa watakaokamatwa wakitupa takataka hovyo.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
16 Aprili, 2016

No comments: