Wednesday, November 04, 2015

DORIS MOLLEL FOUNDATION (DMF) YAANDAA TAMASHA KUBWA LA KUSAIDIA WATOTO NJITI NCHINI, NOV 8 LEADERS CLUB

DSC_0027
Mwenyekiti wa Mfuko wa Doris Mollel Foundation, Bi. Doris Mollel akiwakaribisha wageni mbalimbali na wanahabari wakati wa utambulisho maalum juu ya tamasha linalotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili Novemba 8, katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, uzazi na watoto, Bi. Georgina Msemo na kulia kwake ni Dk. Sonal Peter ambaye ni daktari wa watoto (Pediatrician) kutoka Hospitali ya Agha Khan. (Picha zote na Andrew Chale, Modewjiblog).
Na Andrew Chale, Modewjiblog
[DAR ES SALAAM] Katika kuadhimisha siku ya watoto njiti duniani, Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF) imeandaa tamasha la kwanza na la aina yake kufanyika nchini siku ya Jumapili Novemba 8. 2015 kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni kuanzia majira ya asubuhi mpaka saa 12 jioni huku wasanii mbalimbali wakitarajiwa kushiriki kwa ajili ya kuchangisha fedha za kununulia vifaa vya kusaidia watoto wanaozaliwa na uzito pungufu ama watoto njiti.
Akielezea mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam mapema jana, dhumuni la tamasha hilo ni kuwaleta watanzania pamoja kupata uelewa na mwamko katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa afya na ustakabali wa mtoto njiti ambapo kulingana na takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, takribani watoto 88,128 walizaliwa njiti au wakiwa na uzito mdogo nchini kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 pekee.
“Lengo ni kuhakikisha kupitia Mfuko huu unasaidia watoto njiti hasa kwa vifaa vya kuwawezesha kusaidia maisha yao. Tunataka kufikisha vifaa 10 kwa kila Kanda chache za awali. Karibuni sana watanzania kwa siku ya Jumapili Novemba 8. Kwa kiingilio cha sh 2,000 pekee kama mchango ambapo utapata burudani ya kipekee kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Barnaba Classic, Mwasiti, kundi la The Voice, Miriam, Baraka De Prince, Ruby, Shilole na wengine wengi.” Amebainisha Doris Mollel.
Aidha, Doris amebainisha kuwa, Watanzania watapata fursa maalum ya kuusikia wimbo ulioimbwa na baadhi ya wasanii hao watakaoshiriki katika tamasha hilo.
DMF imeongeza kuwa, baada ya tamasha hilo, kwa kushirikiana na wadhamini pia itatoa vifaa mbalimbali ikiwemo (Suction machines, Oxygen Concentrators na Feeding tubes) hii ni kwa Hospitali za Mikoa nchini ilikuweza kusaidia watoto hao na vifaa hivyo vinatarajiwa kutolewa katika siku ya kilele cha maadhimisho ya mtoto njiti Duniani huku kwa Tanzania ikitarajiwa kufanyika Mkoani Mbeya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, Uzazi na Watoto, Bi. Georgina Msemo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo amezitaka jamii nchini kujitokeza kwa wingi kusaidia wamama wajawazito wakati wa kipindi chote cha ujauzito kwani kusaidia huko kutapunguza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ama njiti.
“Jamii iwe na huruma kwa wamama wajawazito. Kwani haya yote yanatokea kutokana na wamama wengi wanakuwa wanafanya kazi ngumu kutopatiwa huduma muhimu na hata wengine kutokwenda kliniki… hivyo ni jamii ichukue hatua ya kusaidiana na wajawazito kutatua tatizo hili” alieleza Bi Msemo katika taarifa yake hiyo aliyoitoa wakati wa hafla hiyo ya utambulisho wa tamasha la kuchangia fedha za kusaidia watoto njiti.
Wajue Watoto njiti:
Watoto wanaozaliwa kabla ya muda wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa, mfumo wa chakula na mfumo wa fahamu ukilinganisha na watoto waliozaliwa baada ya kutimiza wiki 37 au zaidi wakiwa tumboni mwa mama zao. Watoto njiti pia wapo katika hatari ya kupata matatizo ya kuona, kusikia, kutambua/kiakili na moyo yanayoweza kudumu maisha yao yote. Zaidi ya hapo watoto wanaozaliwa njiti katika nchi zilizo na uchumi duni wapo katika hatari ya kufa mara 10 zaidi ukilinganisha na watoto njiti wanaozaliwa katika nchi zilizoendelea
DSC_0031
Tukio hilo likiendelea.
Tunaweza kupunguza idadi ya njiti
Sababu kuu zinazosababisha hali ya hatari kwa watoto njiti nchini Tanzania na nchi nyingine zenye uchumi mdogo ni maambukizi wakati wa ujauzito, Malaria, VVU, kuzaliwa na uzito mdogo, muda mfupi kati ya uzao mmoja na mwingine na mimba za utotoni. Matunzo sahihi kabla, katikati na wakati wa ujauzito (ikiwemo uzazi wa mpango na huduma wakati wa ujauzito) ni muhimu katika kupunguza kiwango cha uzazi wa watoto njiti. Hata hivyo sehemu kubwa ya sababu zinazofanya watoto kuzaliwa njiti hazijulikani. Hivyo basi tunahitaji kufanyike tafiti zaidi ili kupata uelewa na kudhibiti visababishi vyake.
Tunaweza kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaokufa kutokana na matatizo ya kuzaliwa njiti
Mtoto anayezaliwa njiti sio lazima apewe uangalizi wa karibu (intensive care) na kutumia teknolojia kubwa sana ili aishi. Huduma za gharama nafuu zinazoweza kufanyika ili kuongeza uwezekano wa mtoto mchanga kuishi na kupunguza hatari kwake ya kupata ulemavu wa maisha, ni pamoja na zifuatazo:
1.Antenatal steroids, hizi ni dawa ambazo hutolewa kwa akina mama wanapopata uchungu wa kujifungua kabla ya wakati, katika ngazi za afya zinazostahili, husaiidia kukuza mapafu ambayo hayajakomaa ya mtoto njiti na kuzuia matatizo kwenye mfumo wa hewa ya watoto wachanga.
2.Huduma ya Mama Kangaruu: Hii ni mbinu ya kumbeba mtoto mchanga kwenye kifua cha mama yake wakigusana ngozi kwa ngozi ili kumpa joto na kurahisisha unyonyeshaji. Ni muhimu kuwapatia joto watoto njiti kwa sababu miili yao ni midogo na hupoteza joto haraka, jambo linalowafanya kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa mbalimbali, maambukizi na kifo. Inakadiriwa kuwa mbinu hii ya Mama Kangaruu inaweza kuepusha vifo vya watoto 5,000 kila mwaka hapa Tanzania.
DSC_0048
Baadhi ya wasanii waliokuwapo wakati wa utambulisho huo wakifuatilia kwa makini.
3. Kusaidia watoto kupumua kwa kutumia bag na mask, ni huduma muhimu kwa watoto njiti wenye matatizo ya kupumua. Iwapo huduma hii rahisi ya kusaidia watoto wachanga kupumua inapatikana kwa asilimia 90 ya watoto wanayoihitaji, basi takribani maisha ya watoto wachanga 2,000 yangeweza kuokolewa kila mwaka. Mpango wa Kusaidia Watoto Kupumua (Helping Babies Breathe) ulizinduliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii mwaka 2009 kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya katika ngazi zote, ukiwa na lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na matatizo ya kupumua. Wadau wa afya mbalimbali wameshirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kutekeleza mpango huu.
4.Kumsaidia mama kuanza kunyonyesha mtoto ndani ya saa moja baada ya kujifungua, hii inahusisha pia kumsaidia mama kukamua maziwa kwa ajili ya mtoto na kumpa kwa kutumia kikombe pale inapo lazimu.
5.Kuzuia, kutambua mapema na kutibu maambukizi: utoaji wa huduma inayozingatia usafi wakati wa mama kujifungua (mfano kuosha mikono, uhudumiaji sahihi wa kitovu na ngozi ya mtoto mchanga) ni muhimu katika kuzuia maambukizi kwa mama na mtoto. Dawa za antibiotiki kama vile Amoxicillin zinaweza kutumiwa kutibu nimonia na Gentamicin kwa ajili ya kutibu maambukizi makubwa yanayowapata watoto wachanga.
Zaidi ya hapo, watoto wote wachanga wanahitaji kukaguliwa afya zao ndani ya masaa 24 na baada ya siku 3 ya kuzaliwa ili kuzuia matatizo yanayoweza kutokea na yale ambayo yanaweza kusababisha ulemavu katika maisha yao ya baadaye.
Huduma bora inahitajika wakati wa kujifungua na hususan kwa watoto wachanga wanaozaliwa na uzito mdogo na wale walio wagonjwa.

DSC_0071
Baadhi ya waashiriki hao katika mkutano huo.
“Watoto wachanga wanahitaji kupata huduma muhimu hususan kwa wale ambao wanazaliwa kabla ya muda wao,” anasema Mwakilishi wa Unicef nchini Tanzania Dk. Jama Gulaid.
DMF imetoa pia nafasi ya wazi kwa watanzania kuchangia kiasi chochote kile kupitia M-PESA namba ya kampuni 244444 (Doris Mollel Foundation).
Jinsi ya kuchangia kwa M-Pesa: (1) Piga *150*003# chagua lipa kwa M-pesa (2) Weka namba ya kampuni ambayo ni 244444. (3) Weka kiasi (mfano: Tsh.500, 3200, 7000 na kuendelea kadri ya uwezo wa mchangiaji. (4) Weka namba ya kumbukumbu ambayo ni (2015). Kisha utaweka namba yako ya siri ya M-Pesa (PIN yako ya MPESA) na kisha utabonyeza namba moja kuthibitisha muamala wako na baadae utapokea ujumbe wa maandishi (SMS) kwamba umechangia Doris Mollel Foundation kwenye akaunti michango ya mwaka 2015. (Unaweza kuchangia kiasi chochote mara nyingi uwezavyo.
Aidha, DMF imewashukuru wadhamini mbalimbali wanaoendelea kufanikisha shughuli za kusaidia harakati hizo ikiwemo Vodacom Foundation, Clouds Media Group, Hyatt Regency, NSSF, CBA, NHIF, Coca Cola, Moments productions, Ashton Media, Expo Trading, Viva towers Easy talk, SpiceNet, MillardAyo.com, Modewjiblog na wengine wengi.
DSC_0086
Dk. Sonal Peter ambaye ni daktari wa watoto (Pediatrician) kutoka Hospitali ya Agha Khan akielezea namna ya kuchangia Mfuko huo na kuhamaisha Jamii kujitokeza kwa wingi.
DSC_0096
Wasanii wa kundi la The Voice, Barnaba Classic na wengineo wakiimba kwa hisia wimbo maalum wa kumpa matumaini Mama mjamzito na aliyejifungua mtoto njiti katika kusaidia maisha yake.DSC_0100
DSC_0107
Bi. Doris Mollel akiwapongeza wasanii hao kwa kumuunga mkono katika tukio hilo likiwemo la kuimba wimbo maalum na pia kutumbuiza siku ya Jumapili Novemba 8.2015.
DSC_0129
Mtangazaji wa Chaneli Ten, Said Makalla akiuliza swali kwa Mwenyekiti wa Doris Mollel Bi Mollel (hayupo pichani).
DSC_0144
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, Uzazi na Watoto, Bi. Georgina Msemo (kushoto) akijibu swali la Said Makalla (hayupo pichani).
DSC_0137
DSC_0090
DSC_0088
Kundi la The Voice wakiimba wimbo huo ambapo baadhi ya sehemu walizorekodia ni kwenye wodi ya watoto njiti.

No comments: