Na WMJJWM – DODOMA
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 tayari imetoa shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo zaidi ya 100,000 waliorasimishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 25 Januari, 2026, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga uchumi jumuishi unaowezesha wananchi wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Amesema sekta isiyo rasmi ni mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa kwa kuwaajiri mamilioni ya Watanzania hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hata hivyo, kwa muda mrefu sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kutotambulika kisheria, kukosa mitaji, masoko pamoja na mifumo ya ulinzi wa kijamii.
Kupitia mkakati huo, Serikali imeimarisha zoezi la urasimishaji wa wafanyabiashara ndogondogo ili kuwaingiza katika mfumo rasmi wa kiuchumi, ambapo jumla ya wafanyabiashara 119,595 wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBN–MIS). Aidha, zoezi la utambuzi, usajili na uwezeshaji wa WBN linaendelea katika sekta mbalimbali nchini.
Waziri Gwajima amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1.35 tayari zimetolewa kupitia Benki ya NMB kwa riba nafuu ya asilimia 7 kwa mkopo wa mtu mmoja mmoja, mwanamke au mwanaume. Vilevile, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake unaendelea kutoa mikopo kwa riba nafuu ya asilimia 4. Kupitia TAMISEMI, vikundi zaidi ya 6,000 vimenufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 33.
Aidha, Serikali kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo SIDO, PPRA na TAMISEMI imeendelea kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia mafunzo, leseni na masoko, ikiwemo ushiriki katika zabuni za Serikali. Kwa upande wa taasisi za kifedha, benki zikiwemo NMB, TCB na DCB zimetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa wafanyabiashara waliorasimishwa.
Kwa ujumla, uwekezaji huu wa shilingi bilioni 10.5 umeleta matokeo chanya katika kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo, kuimarisha sekta isiyo rasmi na kuweka msingi wa uchumi shindani na jumuishi. Serikali inaendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kurasimisha biashara zao ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa.








No comments:
Post a Comment