Wednesday, August 19, 2015

NHIF YAOMBWA KWENDA NCHI NZIMA

nh1
Maofisa wa Serikali kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali wakiwa kwenye foleni ya kupima afya zao kwenye banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Serikali Mtandao mjini Arusha.
nh2
Huduma za kupima shinikizo la damu zikiendelea
nh3
Dawati la elimu kwa Umma likiwa kazini
……………………………………………………………………………….
Na Grace Michael, Arusha
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya umeombwa kutekeleza zoezi la upimaji wa afya za wananchi katika Halmashauri zote nchini ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya namna ya kuepukana na magonjwa hayo ili kuliwezesha Taifa kuwa na wananchi wenye afya imara.
Rai hiyo imetolewa na watumishi mbalimbali katika mkutano wa kwanza wa mwaka wa Serikali Mtandao uliofanyika mkoani hapa ambapo Mfuko wa Taifa wa  Bima ya Afya ulitoa huduma za upimaji afya bure katika magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumzia hilo, Godfrey Luguma kutoka Halmashauri ya Wilaya Munduli alisema kuwa ni vyema NHIF ikawa na ratiba ya kuzunguka katika maeneo yote ili fursa hii iwafikie Watanzania wote.
“Upimaji na uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Mifuko hii ikiwemo ya Afya ya Jamii iendelee ili kila mwananchi aweze kutambua hali ya afya yake hatua itakayomuwezesha kuwa na mipango imara ya kimaendeleo,” alisema Bw. Luguma.
Naye Nkide Mwaikuka kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa alitoa mwito kwa wananchi kuhakikisha wanajiunga na utaratibu wa bima ya afya ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati wote.
“Bima ya Afya ni mpango mzuri sana kwa watumishi wa umma na hata wananchi wa kawaida, hivyo NHIF ongezeni elimu kwa wananchi hususan vijijini ili watambue umuhimu wa kuwa au kutumia mpango huu,” alisema Bw. Mwaikuka.
Aidha washiriki wengine wametumia fursa hiyo kupima afya zao huku wakiupongeza Mfuko kwa kuanzisha zoezi hilo kwa lengo la kuhakikisha afya za watanzania zinabaki kuwa bora.
Akizungumzia rai iliyotolewa ya upimaji ndani ya halmashauri zote, Mkurugenzi wa Mifumo Habari wa NHIF, Othman Ali alisema kuwa mpango huo unafanyika katika maeneo mengi ya nchi hii hivyo akawaomba wananchi kutumia fursa hizo wakati zinapokuwa zimejitokeza.
“Tunazo ofisi katika kila mkoa ambazo zinafanya haya majukumu kupitia mpango wa Elimu ya Kata kwa Kata ambapo zoezi la upimaji wa afya kwa wananchi hufanyika,” alisema Bw. Othman.
Post a Comment