Thursday, April 02, 2015

LESENI ZA WACHIMBAJI MADINI 3,449 ZATOLEWA

indexNa Greyson Mwase
……………………………………..
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ngosi Mwihava amesema kuwa jumla ya leseni 3,449 zilitolewa katika mwaka wa fedha 2014/15 kwa wachimbaji wa madini ya aina mbalimbali nchini.
Mhandisi Mwihava aliyasema hayo wakati akielezea mafanikio ya sekta za nishati na madini kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini uliofanyika katika hoteli ya Kunduchi Beach iliyopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam unaoendelea. Lengo la mkutano huo ni kujadili mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Tasisi zake
Alisema kati ya leseni hizo leseni mbili ni za uchimbaji mkubwa, leseni za utafutaji wa madini ni 694, leseni za uchimbaji wa kati ni 21 na leseni za uchimbaji mdogo ni 2,732.
Mhandisi Mwihava alieleza kuwa lengo la kutoa leseni hizo ni kuhakikisha kuwa wachimbaji wanaendesha shughuli za uchimbaji katika maeneo rasmi yaliyopimwa na kuongeza pato la serikali.
Alisema mbali na utoaji wa leseni hizo, wamiliki wa leseni 1,144 wa leseni za utafutaji madini, wamiliki 34 wa leseni za uchimbaji mkubwa na wamiliki 83 wa leseni za uchimbaji mdogo walisajiliwa kutumia mfumo wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao ujulikanao kama Mining Cadastre Portal.
Alisema kuwa mfumo huo unawezesha wamiliki wa migodi hiyo kuhuisha leseni kwa kutumia mtandao badala ya kufunga safari hadi kwenye ofisi za madini.
Mhandisi Mwihava akielezea mafanikio mengine katika sekta ya madini alisema kuwa mwezi Desemba, 2014 kampuni ya uchimbaji madini ya Resolute (T) Limited ilikabidhi miundombinu yote ya mgodi wa Golden Pride kwa Chuo cha Madini Dodoma ambayo itatumia kufundishia wanafunzi wa chuo hicho kwa vitendo.
Aliongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi mbili za Kanda na nne za Afisa Madini Mkazi ambazo zinafanya kazi.
Alitaja ofisi hizo kuwa ni pamoja na Kanda ya Ziwa Nyasa – Songea, Kanda ya Ziwa Viktoria Mashariki – Musoma, Ofisi za Madini Mkazi zilizopo Bariadi, Moshi, Nachingwea na Njombe.
Wakati huo huo akielezea mafanikio ya sekta ya nishati, Mhandisi Mwihava alisema kuwa hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi 1 ulikamilika kwa asilimia 84 ambapo mitambo yote minne pamoja na mitambo ya kupooza injini imeshafungwa kwenye eno la mradi na kusisitiza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema Juni mwaka huu.
Aliongeza kuwa mradi wa ujenzi wa bomba la gesi umekamilika kwa asilimia 97 na kuongeza kuwa mara baada ya ukamilishwaji wake wananchi wataanza kupata umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu.
“ Pamoja na hayo, hadi kufikia Februari, 2015 jumla ya wateja wapya 131, 180 walio ndani na nje ya gridi ya taifa wameunganishwa na umeme ambayo ni sawa na asilimia 75 ya lengo la Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa mwaka ambalo ni kuunganisha wateja 175,000. “ Alisisitiza Mhandisi Mwihava
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa kampuni ya maendeleo ya joto-ardhi Tanzania ambayo ilianza kazi yake rasmi tangu Julai, 2014 na ukamilishwaji wa rasimu ya sera ya nishati na mafuta ambazo ziko kwenye hatua ya kuwasilishwa kwenye baraza la Mawaziri

No comments: