Mgeni rasmi katika mbio hizo ,Waziri mkuu Mstaafu ,Fredirck Sumaye akiingia uwanjani huku akihitimisha mbio za km 21 .
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini.
WANARIADHA wa Tanzania Joseph Theofily wa klabu ya riadha ya Holili ya mkoani Kilimanjaro na Failuna Abdi wa klabu ya riadha ya Winning Spirit ya jijini Arusha wamefanikiwa kupeperusha vyema Bendera ya taifa baada ya kuibuka washindi wa kwanza katika mbio za kimataifa za
Ngorongoro Marathoni kwa upande wa wanaume na wanawake.
Mwanariadha Theofily alifanikiwa kumaliza mbio za km 21 akitumia muda wa saa 1:03:09 na kujinyakulia kitita cha sh Mil, 1. mbele ya wakongwe wengine kutoka nchi za Kenya ,Uganda na Malawi huku Gabriely Gerald wa klabu ya Winning Spirit ya jijini Arusha akishika nafasi ya pili akimaliza mbio akitumia saa 1:03:36 na kujinyakulia kitita cha sh laki 5.
Emanuel Giniki alifanikiwa kushika nafasi ya tatu na kujinyakulia zawadi ya sh 250,000,nafasi ya nne ikichukuliwa na Ezekiel Therop huku mwanariadha Mohamed Msenduki wa klabu ya Wining Spirit ya jijini Arusha akimaliza nafasi ya tano.
Mwanariadha wa kike Failuna aliyerejea hivi karibuni kutoka nchini Brazil kushiriki mashindano ya mbio za Km 15 ambazo alifanikiwa kumaliza mbio hizo katika nafasi ya saba,aliwaongoza wakongwe kama Banuelia Bryton ,Marry Naali Jackline sakilu na Catherine Range akimaliza mbio katika nafasi ya kwanza kwa kutumia muda wa saa1:10:25.
Failuna aliyejinyakulia zawadi ya kitita cha kiasi cha sh Mil,1. alifuatiwa kwa karibu na mpinzani wake Nathalia Elisante aliyetumia muda wa 1:14:40 na kuzawadiwa kitita cha sh 500,000 huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Magdalena Crispine aliyetumia muda wa 1:15:56, nafasi ya nne na tano ikienda kwa Anjelina Tsere na Merry Naali.
Mbio za kimataifa Ngorongoro Marathoni zinafanyika zikiwa na lengo la kuwawezesha watoto wa jamii ya kimasai kupata elimu ikiwemo kumalizia shule ya Endulen iliyoko Ngorongoro na kutangaza urithi wa utalii kupitia hifadhi ya taifa ya Ngorongoro huku ikishirikisha pia mbio za Kilomita tano kwa wafanyakazi wa taasisi mbalimbali pamoja na Km 2.5 kwa wanafunzi. |
Comments