VIJANA WAMESHAURIWA KUJALI AFYA ZAO KWA KUJIUNGA NA MFUKO WA AFYA WA JAMII (CHF)

1
Mhamasishaji kutoka Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa akifungua semina ya vijana wa Kata ya Lepurko na Sepeko kuhusu Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo katika Kata ya Lepurko Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha. Kushoto ni Afisa Vijana kutoka Wizara hiyo Bi. Amina Sanga, wa kwanza kulia ni Afisa Mtendaji Kata ya Lepurko Bw. Sambeta Moikan na wapili kulia ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele.
2
Afisa Maendeleo ya Vijana Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Bi. Mesha Singoyo kulia akifafanua jambo wakati wa semina ya Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika Kata ya Lepurko Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha.
3
Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga kulia akimsikiliza kwa makini kijana kutoka Kata ya Lepurko aliyekua akielezea kuhusu ufahamu juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wakati wa semina ya Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika Kata ya Lepurko Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha.
4
Mhamasishaji kutoka Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa akiwaonyesha vijana wa Kata ya Lepurko na Sepeko mfano wa andiko la mradi linavyotakiwa kuwa wakati wa semina ya vijana wa Kata hizo katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha.
6
Dkt. Machuman Kiwanga kutoka Hospitali ya Wilaya ya Monduli akiwaonyesha vijana wa Kata ya Lepurko na Sepeko kadi za uanachama wa mfuko wa afya wa jamii (CHF) kuwahamasisha vijana hao kujiunga na mfuko huo kupata huduma za afya kwa bei nafuu wakati wa semina ya vijana katika kata ya Lepurko Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha.
7
Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele akitoa mada wakati wa Semina ya Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa vijana wa Kata ya Lepurko na Sepeko katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha.
Picha na: Genofeva Matemu – Maelezo, Monduli
………………………………………………………
Vijana wameshauriwa kujiunga na Mfuko wa afya wa jamii (CHF) unaotoa huduma rafiki ya afya katika jamii ili kuweza kuwa na afya bora itakayopelekea kuleta uchumi imara ndani na nje ya jamii ya kimasai.
Hayo yamesemwa na Dkt. Machuman Kiwanga kutoka Hospitali ya Wilaya ya Monduli wakati wa semina ya vijana wa Kata ya Lepurko na Sepeko kuhusu Ujasiriamali, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo katika kata ya Lepurko Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha.
Akifafanua masuala ya afya katika Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007 Dkt. Kiwanga amesema kuwa kama vijana watajitambua na kuhimili mihemko ya miili yao watafanikiwa kupunguza tatizo la magonjwa ya zinaa likiwemo ngonjwa la ukimwi linalowakumba vijana wengi wakiwemo wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 20 kutokana na ngoma ya esoto inayomuandaa mtoto wa kike kabla ya kufunga ndoa pamoja na ukeketaji wa watoto wa kike. 
“Serikali ina mpango wa Kujenga zahanati katika kila Kijiji na Vituo vya Afya katika kila Kata ikiwa ni mkakati wa kuboresha afya haswa kwa vijana katika masuala ya uzazi salama na ukimwi ili kuweza kuwa na uchumi imara katika jamii zetu” amesema Dkt. Kiwanga.
Aidha Mhamasishaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa amesema kuwa vijana wa Monduli wamepata fursa ya pekee ya kupata elimu ya afya uzazi na ukimwi itakayowawezesha kubadilika na kujali afya zao kwa kuachana na mila na desturi zinazowakosesha fursa za kiujasiriamali.
Bibi Riwa amesema kuwa ujana ni kipindi cha mpito ambacho kama kitatumika vibaya kitapoteza ndoto za vijana wengi hivyo kuwataka vijana wa Monduli kuwa na dira inayojali maamuzi yao kama vijana na kuwaongoza katika maisha bora kwa kutumia nguvu walizonazo.
Naye mshiriki wa semina hiyo Bibi. Naparakwo Leiio ameishukuru serikali kuwakumbuka vijana wa Monduli kwa kuwafikia na kuwapa elimu ambayo hawakuwa nayo hivyo kuhaidi kutumia elimu aliyoipata katika semina hiyo kuhamasisha vijana wengine katika vikundi vyao na kujenga umoja kati yao kwani umoja ndio suluhisho la unyanyasaji na ngao ya kuondokana na umasikini.

Comments